Serikali Yaitaka Bodi TTCL Kujikita Kwenye Ubunifu wa Kiushindani

Serikali Yaitaka Bodi  TTCL  Kujikita Kwenye Ubunifu wa Kiushindani
Serikali imeaiambia bodi mpya ya wakurugenzi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kuacha kuremba, badala yake wajikite kwenye ubunifu huku wakijielekeza kwenye ushindani dhidi ya kampuni zingine za mawasiliano nchini.

“Nataka bodi mjue tunakwenda wapi katika kampuni hii, lakini pia tunahitaji kufanya kazi kwa juhudi kushindana na kampuni nyingine za simu,” alisema Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akizindua bodi hiyo jana ambapo aliongeza kuwa; “Mhakikishe mapato makubwa yanatoka kwenye data, halikadhalika mnapaswa mjue nguvu yenu iko wapi maana tusipojibu maswali haya hatuwezi kufanya ushindani na kampuni nyingine.”

TTCL ambayo ilibaki nyuma kiushindani kwa muda mrefu, hivi sasa imeibuka kwa nguvu baada ya Serikali kuamua kuirejesha mikononi mwake kutoka kwenye ubia baina yake na Airtel.

Hata hivyo, Profesa Mbarawa alisema asingependa kuiona ikijivutavuta katika hali ya sasa ya soko la mawasiliano ambalo linahitaji ubunifu na mikakati mathubuti ili kuweza kumiliki soko.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa TTCL, Omary Nundu alisema tangu ateuliwe wamefanya mambo mengi hadi sasa ikiwamo kuifufua kampuni hiyo, kushirikiana na wadau wengine wa mawasiliano pamoja na kuanzisha huduma ya utumaji na upokeaji wa fedha maarufu kama TTCL Pesa.

Nundu alisema mwaka 2016, TTCL ilipata Sh0.21 bilioni katika soko na mwaka huu wanatarajia kupata Sh0.3bilioni na kwamba wanatarajia faida ya zaidi ya Sh40 bilioni ifikapo 2022 baada ya makato ya kodi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad