Serikali Yamjia juu mtumishi Aliyeshinda CCM

Serikali Yamjia juu mtumishi Aliyeshinda CCM
Serikali mkoani Morogoro imemtaka mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya Mvomero, Salvatory Richard aliyeshinda nafasi ya Uenyekiti wa Wazazi wa CCM wilayani humo kuchagua utumishi wa umma ama siasa.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Clifford Tandari amesema haiwezekani kwa mtumishi wa umma kutumikia nafasi ya kisiasa kwani sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma zinakataza.

"Tulikuwa na kikao asubuhi na tumeiagiza Halmashauri ya Mvomero kumchukulia hatua stahiki mtumishi huyo kwani kanuni na taratibu za Serikali haziruhusu mtumishi kutumikia nafasi hizo mbili," amesema.

Tandari amesema mtumishi huyo ataeleweshwa taratibu za utumishi wa umma zilivyo ili aamue kama atabaki serikalini ama ataenda kutumikia siasa.





Katibu tawala huyo amewaonya watumishi wa Serikali mkoani humo kuhakikisha wanapitia na kuelewa kanuni za utumishi wa umma vizuri ili kuondoa migongano isiyo ya lazima.

"Tumekuwa tukitoa elimu mara kwa mara kwa watumishi wetu kuhusu sheria na kanuni za utumishi wa umma lakini sijui kwa nini hawazingatii," amesema Tandari.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mvomero, Florent Kyombo amesema tayari wameshaanza kuchukua hatua katika kushughulikia swala hilo.

"Leo tumewaandikia CCM barua ili kwanza tupate uthibitisho wa maandishi kwamba ni kweli mtumishi wetu amechaguliwa katika nafasi husika,” amesema.

Amesema CCM wakishathibitisha kuhusu mtumishi huyo ndipo halmashauri itakapoanza utaratibu wa kumtaka aamue kuacha kazi au aombe likizo bila malipo ili aweze kutumikia kwanza nafasi aliyoipata.

Kyombo amesema halmashauri itafuata sheria, kanuni na taratibu za kuongoza Serikali katika kushughulikia suala la Richard.

Katibu wa Wazazi wa CCM wilayani Mvomero, Ally Castro amesema kwa upande wa chama Richard alikuwa na haki ya kuchaguliwa na wanachama wametimiza wajibu wao.



"Katika chama tunahimizwa kuchagua kiongozi mwenye kipato halali na huyu ana kipato halali lakini pia CCM ni ya wakulima na wafanyakazi, sasa shida iko wapi," alihoji Castro.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad