Serikali Yatoa Tamko Zito Mali za Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC)

Serikali Yatoa Tamko Zito Mali za Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC)
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba ameagiza kupitiwa upya mali zote zilizokuwa zikimilikiwa na Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC). 

Ametoa agizo hilo akizindua bodi mpya ya wakurugenzi ya nafaka na mazao mchanganyiko mjini hapa.

Dk Tizeba amesema mali zote za NMC ambazo hazikuuzwa zitamilikiwa na bodi hiyo.

Amewataka kuingia upya mikataba  na kuisimamia ili kuondoa ubabaishaji uliokuwa ukifanya na baadhi ya watu waliojimilikisha mali za Serikali kama vile  maghala na mashine.

Waziri amesema lengo la Serikali kuanzisha bodi hiyo ni kuhakikisha inasimamia pamoja na mambo mengine mali ambazo hazikubinafsishwa zilizoko Mwanza, Iringa, Arusha na Dodoma. 

“Changamoto zilizojitokeza wakati wa NMC na Gapex lazima bodi ikabiliane nazo kwa umakini na kuzifanyia kazi ili zisijitokeze tena,” amesema.

Dk Tizeba ameagiza bodi hiyo kujihusisha na usambazaji wa pembejeo za kilimo na usindikaji ili kuondoa matatizo ya upatikanaji wake na kuongeza thamani za mazao ya wakulima. 

Kaimu mkurugenzi wa bodi hiyo, John Maige amesema watashirikiana na wakulima na wadau wengine na kwamba, watafanya kazi kwa ushindani kama taasisi huru ya kiuchumi.

Amesema bodi itahakikisha inatumia mali ilizopewa na Serikali kujenga uwezo wa kimtaji.

Bodi ina uwezo wa kununua mazao mchanganyiko kutoka kwenye vikundi vya wakulima katika mikoa ya  Iringa, Ruvuma, Songwe, Mbeya na Njombe.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad