Zitto amebainisha hayo kupitia ukurasa wake wa Facebook baada ya kutazama nyumba yake ya kwanza iliyoteketea kwa ajali ya moto mwishoni mwa wiki iliyopita.
"Sikudhani kabisa kuwa naweza kuumizwa na kupata uchungu kwa tukio kama hili na ninajiuliza huu uchungu ni wa nini? Kumbe ni uchungu wa nyumba ya kwanza. Nawafikiria wananchi wenzangu wanaobomolewa nyumba zao bila fidia, na wengi ni nyumba zao za kwanza na pekee. Uchungu wao nausikia. Hasira zao nazihisi" Zitto ameandika.
Ameongeza kuwa "Nafikiria wanaobomolewa maeneo ambayo yamekuwa sehemu ya maisha yao na kuwapa kipato na familia zao. Nausikia uchungu wao.Sio uchungu wa nyumba ya kwanza. Uchungu wa kupoteza kabisa walichonacho na pengine kupoteza matumaini ya maisha"
Pamoja na hayo Zitto amesema kuwa ameridhika kwamba kilichotokea kwenye nyumba yake kuungua moto ni ajali ya kawaida na wala watu wasichukulie kwa muktadha wa matukio yanayoendelea nchini kwetu hivi sasa.
"Ni ajali na funzo ni kuchukua tahadhari zaidi. Hasara ni kubwa sana lakini muhimu ni kuwa maisha yanaendelea na Mungu ataleta uwezo wa kuendeleza mengine. Nilipata salaam kutoka kwa watu wengi na napenda kuthibitisha kuwa ni ajali tu" Zitto.
Mbali na hayo Mh. Zitto Kabwe amesema kuwa nyumba yake imeungua siku moja baada ya yeye kuondoka Kigoma na akiwa njiani kuelekea nchini Kenya ndipo alipatiwa taarifa kuhusu ajali hiyo.
"Ajali imetokea siku moja tu baada ya mimi kutoka Kigoma, Septemba 15 , 2017. Hata hivyo muda wote wa siku 2 nikiwa nje ya Kigoma, sikupata hisia kabisa. Labda ni kwa sababu ya safari yangu ya Kenya ambayo nayo haikuwa ni kwa jambo la kawaida" Zitto.
Aidha Mh Zitto ameongeza "Leo asubuhi nimeamka na kurudi kutazama nyumba hii. Imekwisha yote nimezunguka zaidi ya mara 3 kutazama gofu lile lile nililotazama jana baada ya kufika. Nimechungulia chumba nilichokuwa nalala zaidi ya mara moja. Nipo kama mwendawazimu" alisisitiza Zitto Kabwe.
Nyumba ya Zitto Kabwe iliyoungua huko Mwandiga mkoani Kigoma inadaiwa ndiyo nyumba yake ya kwanza baada ya kupata ridhaa ya kuwa mbunge