SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amewatadharisha wabunge kuwa makini na usalama wao mahali popote wanapokwenda kufuatia matukio mengi ya uhalifu nchini. Akizungumza muda mfupi leo Ijumaa, Septemba 15, kabla ya kuahirishwa kwa Bunge, Ndugai aliwataka wabunge kutokaa sana katika mabaa.
“Yaani tuchukue hatua tu katika maisha yetu, kama mnavyosikia matukio ni mengi katika nchi yetu. Ni vizuri usalama unaanza na wewe mwenyewe kwanza,” amesema.
Amesema vyombo vya usalama vinavyowalinda vinakuwa vinaongezea kidogo na kuwataka kutazama nyendo zao za namna ambavyo wanaishi.
Spika Ndugai: Wabunge Tuchukue Hatua za Usalama Wetu
“Kwa wale tuliozoea tunarudi nyumbani saa saba usiku, basi tuanze kurudi mapema kidogo. Lakini pia tuangalie usalama wa familia zetu na tuwaambie wapigakura, naona siku hizi watoto wanapotea, watoto wanauawa,” amesema.
Amewataka wabunge kuwapelekea ujumbe huo wananchi kuwa wawe makini na watoto wao wakati wa kwenda shule na maeneo mengine kwa kuhakikisha wanajua mtu anayewapeleka shule na kuwachukua.
Aliwataka wabunge kuendelea kumuombea Tundu Lissu na wale watakaopata nafasi ya kwenda kumuona jijini Nairobi wampelekee ujumbe.
Amesema pia wabunge wawaombee wenzao ambao wamekwenda kumuuguza mbunge huyo. Ushauri huo umekuja siku chache baada ya Lissu kujeruhiwa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake Area D mjini Dodoma.