SUTI ya Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, inayoonekana kuzidi kipimo cha kawaida, imezua mjadala katika mitandao ya kijamii.
Maalim Seif alivaa suti hiyo mwanzoni mwa wiki alipokwenda kumjulia hali Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, aliyelazwa hospitalini jijini Nairobi, Kenya.
Lissu amelazwa katika Hospitali ya Nairobi baada ya kupigwa risasi tano na watu wasiojulikana wakati akiwasili nyumbani kwake, Area D, mjini Dodoma Septemba 7, akitokea bungeni.
Katika picha aliyopiga kiongozi huyo akiwa pamoja na watu wengine, mke wa Lissu na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Maalim Seif alionekana amevaa suti yenye vipimo vikubwa tofauti na ilivyozoeleka, hali iliyozua gumzo katika mitandao ya kijamii.
Katika picha hiyo pia anaonekana aliyekuwa mgombea mwenza wa Urais wa Ukawa katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Juma Duni Haji.
Katika picha hiyo, Maalim Seif alionekana pia ameshika fimbo, huku suti aliyovaa yenye rangi ya kijivu ikiwa imemzidi kwa ukubwa.
Picha hiyo ya Maalim Seif imekuwa kwenye mjadala katika makundi mbalimbali ya kijamii hasa ya mtandao wa WhatApp huku wengi wakijiuliza ni kitu gani kimemkumba kiongozi huyo mkubwa ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar.
Nipashe, lilifanya jitihada za kumtafuta Maalim Seif, ili aelezee undani wa suti aliyovaa, lakini simu yake haikupatikana.
Wananchi mbalimbali walitoa maoni yao kwenye mitandao pamoja na WhatsApp, Facebook na Instagram wakihoji ni fundi gani aliyemshonea suti hiyo Maalim Seif.
Moja ya mtu aliyechangia mjadala huo aliandika "Aliyemshonea hiyo suti Mungu anamuona!"
Wengine waliandika "uwiii hiyo ni suti ya karne", "hii suti haijapata kutokea jamani" na "mbona kubwa au fundi hakutaka kitambaa kibaki?"
"Fundi aliyeshona hii suti mwambieni anywe soda kwa hela yake," aliandika mchangiaji mwingine na wengine wakaandika "duuu huyu fundi Mungu anamwona kwa alichokifanya" na "hiyo fashion ya suti haijapata kutokea".
Tukio kama hilo la Maalim Seif, liliwahi kumtokea kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Steven Wasira baada ya koti alilovaa kufungwa vishikizo vilivyopishana mwaka 2015.
Wasira alifikwa na mkasa huo akiwa katika Sherehe za Utume zilizoandaliwa na Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA).
Wakati wa upigaji picha, alionekana vishikizo vya koti lake vikiwa vimepishana.
Suti ya Maalim Seif Iliyozidi Kipimo Yaleta Gumzo Mitandaoni
1
September 29, 2017
Tags
Duh! jamani dhambi! kwa nini lakini? Kashonesha au 'NITUNGULIE ILEE'
ReplyDelete