Waandaaji wa Fiesta, Kampuni ya Clouds Media Group wamesema hakuna mtu aliyezuiwa kuingia katika tamasha hilo.
Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds, Ruge Mutahaba amesema wao wanafanya biashara hivyo hawawezi kuzuia mtu kuingia kwenye tamasha hilo.
Fiesta kwa msimu huu ilizinduliwa jana Jumamosi jijini Arusha. Tamasha hilo linafanyika kwa mwaka wa 18 na limekuwa likiwashirikisha wasanii wa ndani na kimataifa.
Ruge ametoa kauli hiyo alipotakiwa na Mwananchi kuzungumzia tweet ya mwanamuziki mkongwe wa Bongo Fleva, Hamis Mwinjuma maarufu MwanaFA. Akim-tag rafiki yake, kupitia ukurasa wake wa Twitter, MwanaFA aliandika: “Unapogundua sio tu huruhusiwi kuperfom bali hata kwenda kuangalia burudani kwenye tamasha lolote linalohusisha ile kampuni @AyaTanzania.”
Baadaye aliandika tena: “Kwa hiyo haturuhusiwi mpaka tusamehe bilioni 2.2 taslimu fedha za kiTanzania? bro, tumekwisha.”
Tamasha la Fiesta msimu huu linadhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Tigo, ambayo nayo imesema hakuna aliyezuiwa.
“Hakuna anayezuiwa kuingia kwenye tamasha. Hatukumzuia yeyote mwenye tiketi kuingia tamashani,” amesema Woinde Shisael, meneja mawasiliano wa Kampuni ya Tigo.
Taarifa zilizopo zinasema msanii huyo hakuzuiwa kama habari zinavyosambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Inaelezwa akiwa ameambatana na watu waliokuwa na mwaliko wa kukaa eneo lililotengwa kwa ajili ya watu mashuhuri (VIP) yeye alizuiwa kwa kuwa hakuwa amealikwa.
MwanaFA na msanii mwenzake Ambwene Yesaya maarufu AY wamefungua kesi mahakamani ikihusisha kampuni ya Tigo wakitaka kulipwa fidia ya Sh2.1 bilioni kwa kukiukwa Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki, kwa kutumia kazi zao (nyimbo) kama miito ya simu bila ridhaa wala makubaliano nao.