Taarifa ya Serikali Kuhusu Upanuzi wa Barabara ya Morocco Mwenge
0
September 02, 2017
Dar es Salaam, Septemba 1, 2017: Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo (JICA), imeipatia Tanzania ruzuku ya Yen milioni 69 sawa na Shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina wa awamu ya pili ya mradi wa upanuzi wa barabara ya New Bagamoyo, kuanzia Morocco hadi Mwenge, Jijini Dar es Salaam.
Makubaliano ya msaada huo yametiwa saini Septemba 1, 2017, Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) kwa niaba ya Serikali, Balozi wa Japan nchini Tanzania Masaharu Yoshida na Mwakilishi Mkazi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Japani (JICA), Satoru Matsuyama.
Tukio hilo limekwenda sambamba na kuingia makubaliano kuhusu muda wa kukamilisha mradi huo pamoja na kupeana taarifa ya namna mradi huo utakavyotekelezwa.
Mradi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 4.3 utahusisha barabara yenye njia nne pamoja na kuanza kwa awamu ya nne ya barabara itakayotumiwa na mabasi ya mwendo wa haraka (BRT phase IV).
Akizungumza baada ya kutiwa saini wa makubaliano hayo, Dkt. Mpango amesema kuwa barabara hiyo ikikamilika itasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya msongamano wa magari kutoka na kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Ameishukuru Japan kwa msaada huo wa awamu ya pili ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo katika awamu ya kwanza, Japan ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 99.5. kujenga barabara ya njia nne katika kipande cha kilometa 12.9 kutoka makutano ya barabara ya Tegeta na makutano ya barabara ya Mwenge.
“Si mara ya kwanza kwa Japan kuisaidia Tanzania, wanajenga barabara za juu katika makutano ya Tazara, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Dodoma hadi Babati mkoani Manyara (km 188.15), Tunduru-Mangaka – Mtambaswala (km 202) na barabara ya Iringa hadi Dodoma (259.9)” alisisitiza Dkt. Mpango.
Alisema kuwa upanuzi wa barabara ya Bagamoyo si tu kwamba itapunguza msongamano wa magari Jijini Dar es Salaam lakini pia utaunganisha Jiji na Bandari ya Bagamoyo ambayo ni muhimu kwa ajili ya usafirishaji wa watu, bidhaa na huduma kutoka Jijini, mikoa ya Pwani na maeneo mengine ya nchi.
Balozi wa Japan, Mhe. Masaharu Yoshida ameeleza kuwa kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa awamu ya pili ya barabara ya Morocco hadi Mwenge kumekuja baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza iliyohusisha ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Tegeta hadi Mwenge ili matokeo ya mradi huo yaweze kuonekana dhahiri.
Ameahidi kuwa baada ya kukamilika kwa usanifu wa kina wa barabara hiyo, Serikali ya Japan kupitia JICA, itasaini mkataba wa kuanza ujenzi huo Mwezi Juni mwakani.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Bw. Satoru Matsuyama, amesema Japan imeamua kufadhili mradi huo baada ya utafiti kuonesha kuwa Barabara ya Bagamoyo ndiyo yenye msongamano mkubwa wa magari ambapo inakadiriwa kuwa magari 52,000 yanapita kila siku katika barabara hiyo.
Alielezea matumaini yake kwamba mradi huo utakapo kamilika utasaidi kukuza shughuli za kiuchumi katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa ndicho kitovu cha biashara kwa maeneo mengine ya ndani ya nchi na kimataifa na kuwaomba wataalamu pamoja na TANROADS kuharakisha usanifu huo wa kina.
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini-TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale, amesema kuwa ujenzi wa barabara hiyo hautahusisha ubomoaji wowote wa makazi ya watu wala majengo ya biashara.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Tags