Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), imebadilisha tarehe ya kufanyika uchaguzi wa marudio wa Urais ambao sasa utafanyika Oktoba 26.
Awali, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Oktoba 17, siku 60 baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya uchaguzi wa awali uliompa ushindi Uhuru Kenyatta wa Chama cha Jubilee.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Tume hiyo, Wafula Chebukati imeeleza uamuzi huo umefikiwa ili kuipa IEBC muda wa kujiandaa zaidi na hasa katika masuala ya teknolojia.
“Ni dhahiri kuwa, kufutwa kwa uchaguzi kumeleta athari na hasa kwenye teknolojia itakayotumika,” amesema.
Chebukati amesema, “Ili kuhakikisha tume inajiandaa kuleta uchaguzi wenye viwango vinavyohitajika na Mahakama ya Juu, tunapenda kuujulisha umma na wadau wote kuwa uchaguzi mpya utafanyika Alhamisi Oktoba 26.”
Tume pia imesema itayapitia maagizo ya Mahakama ya Juu kuhusu uchaguzi wa marudio.
Kenya Septemba Mosi iliweka historia baada ya Mahakama ya Juu kufuta matokeo ya Urais yaliyompa ushindi Rais Kenyatta kuwa madarakani kwa muhula wa pili.
Mgombea wa Muungano wa Nasa, Raila Odinga alifungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Agosti 8, akisema ulitawaliwa na udanganyifu ikiwemo kuchezewa mitambo ya kujumlishia matokeo.
Katika uchaguzi wa Agosti 8, Kenyatta alitangazwa mshindi kwa kupata kura 8,203,290 sawa na asilimia 54.27, huku mpinzani wake Odinga akipata kura 6,762,224 sawa na asilimia 44.74.