Matumaini ya kufanyika uchaguzi wa marudio kwa kura ya urais Oktoba 26 yamefifia baada ya jana wawakilishi wa vyama vya Jubilee na muungano wa Nasa kushindwa kukubaliana kuhusu masuala muhimu katika mazungumzo ya maandalizi.
Muungano wa Nasa ulipinga hatua ya Jubilee kushinikiza kupitishwa miswada yenye lengo la kufanyia marekebisho sheria za uchaguzi na ikatangaza mgomo mkubwa kila Jumatatu na Ijumaa kuanzia wiki ijayo katika kile ilichodai ni juhudi za “kuikomboa nchi kutoka Jubilee”.
Wakionekana kutoshangazwa na mgomo wa wapinzani, wabunge wa Jubilee bungeni walifupisha muda wa kuanza kutumika Sheria ya Uchaguzi (Marekabisho) za mwaka 2017 ambazo pamoja na mambo mengine, zinataka kupunguza mamlaka ya mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC), na kuwaadhibu wagombea watakaojitoa kushiriki uchaguzi wa marudio.
Pia mswada unapendekeza kuchukuliwa hatua kali kisheria dhidi ya maofisa watakaokataa kutia sahihi fomu 34A na 34B, ikiwamo kutumikia kifungo cha jela miaka 5. Mahakama imenyimwa mamlaka ya kubatilisha ushindi wa rais ukipendekeza kura zilizoko kwenye masanduku zihesabiwa upya, kando na sheria zingine.
Ilipendekezwa sheria hizo ziwe zimeiva na kuanza kutumika baada ya siku 14 lakini wabunge walibadili muda wa mwisho wa marekebisho hayo kutumika iwe siku moja tu.
IEBC yenyewe ikielezea namna ilivyojiandaa kwa uchaguzi wa marudio kama ulivyopangwa, imesema mapendekezo ya marekebisho hayo siyo ya lazima kwa sababu mambo yote ambayo tume ilikuwa na uhuru kusimamia majukumu yake.
Tume imesema sheria za sasa zinatosha kuendesha uchaguzi wa marudio wala hawahitaji nyingine. "Tumetambua dosari zetu na maeneo yanayopaswa kushughulikiwa na kuimarishwa. Hatuhitaji sheria nyingine kuendesha uchaguzi wa Oktoba 26, 2017," alisema Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati Alhamisi alipozungumza na waandishi wa habari juzi katika Ukumbi wa Bomas of Kenya baada ya mkutano kati ya tume hiyo, muungano wa Nasa na Jubilee kuvunjika kutokana na kutokuwepo makubaliano.
Chebukati alisema makosa yaliyotajwa na Mahakama ya Juu wakati wa kubatilisha uchaguzi wa urais wa Agosti 8, hayakutokana na upungufu wala ukosefu w sheria. "Hitilafu zilizotajwa hazikutokana kwa sababu ya ukosefu wa sheria. Tumerekebisha 'nyumba yetu' na ninalihakikishia taifa kuwa Oktoba 26 sharti tufanye uchaguzi kama ilivyoagiza mahakama," alisema.
Juhudi za kujadili kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo juzi hazikuzaa matunda baada ya ujumbe wa Nasa ukiongozwa na Seneta wa Siaya James Orengo, kuondoka katika ukumbi wa mkutano huo kwa kile walichodai ni kughadhabishwa na mswada wa Jubilee bungeni wa kutaka kubadilisha sheria za uchaguzi.
"Ifahamike wazi sipingi mswada huo, lakini kwa sasa tuna sheria za kutosha," alisisitiza Chebukati.
Kuhusu uwezekano wa baadhi ya wagombea kujiondoa kushiriki uchaguzi huo wa marudio Chebukati alisema hajapokea barua wala taarifa yoyote ya kujitoa kushiriki kutoka kwa mgombea yeyote wa kiti cha urais.
"Tumeshachapisha majina ya wagombea wawili wa kiti hicho katika Gazeti la Serikali, na hakuna aliyeniletea barua akisema hatashiriki uchaguzi," alisema.
Uchaguzi wa marudio utawashirikisha wagombea wawili tu, Rais Uhuru Kenyatta ambaye anapeperusha bendera ya Jubilee, na aliyewa kuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kwa tiketi ya muungano wa Nasa.
Mwenyekiti huyo aliwaambia waandishi wa habari kwamba katika mkutano mwingine ujao hatahitaji wawakilishi bali wagombea urais wenyewe yaani Uhuru na Raila.
"Mkutano wa leo (Alhamisi) hatujaafikiana kwa sababu ya mswada ulioko bungeni. Katika mkutano ujao wa upatanisho, tutahitaji wagombea wa urais wenyewe kuhudhuria," alieleza.
Jubilee
Viongozi wa Jubilee wamesema mswada wa kubadilisha sheria za uchaguzi uliowasilishwa bungeni umewakasirisha Nasa kwa sababu umefunga mianya yote ya kususia kushiriki uchaguzi wa Oktoba 26.
Jubilee inasema Nasa wanataka kuzua mvutano kwa sababu wametambua mswada huo unawashurutisha kushiriki uchaguzi kwa kuwa umeondoa vikwazo vyote vilivyotajwa na Mahakama ya Juu wakati ikitoa maelezo yake kwa kina ya kufutilia mbali ushindi wa Rais Kenyatta.
"Wenzetu wameghadhabika kwa sababu tumeziba mianya yote ya kutoepuka kushiriki uchaguzi wa Oktoba kupitia mswada huo," alisema Seneta wa Elgeiyo Marakwet, Kipchumba Murkomen nje ya Ukumbi wa Bomas of Kenya baada ya mkutano kuvugika.
"Tunachotaka ni uchaguzi wa huru, haki na wazi," akaongeza Seneta huyo.
Nasa inashikilia kuwa haitashiriki uchaguzi huo wa Oktoba 26, hadi pale IEBC itakapofanya mabadiliko ikiwamo kumfurusha Mkurugenzi wake Ezra Chiloba na maafisa wengine. Pia hawataki kuhusishwa kwenye uchaguzi huo kampuni ya mawasiliano ya Safaricom, ya uchapishaji karatasi za kupiga kura Al-Ghurair (Dubai) na Safran Morpho (Ufaransa).
"Sisi tumejiandaa kushiriki uchaguzi huo, tunajua wenzetu hawajajiandaa ndio maana wana sarakasi nyingi," alieleza Murkomen.