Waajiri 126 katika jiji la Arusha wanategemewa kufikishwa mahakamani mwezi ujao Oktoba mwaka huu kwa kosa la kukatisha michango ya wafanyakazi wao kwenye Shirika la Hifadhi ya Jamii mkoani Arusha.
Meneja Kiongozi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii mkoani Arusha, Frank Magu Maduga.
Meneja Kiongozi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii mkoani Arusha, Frank Magu Maduga amesema kuwa kuna makampuni zaidi ya 100 ambayo yatafikishwa mahakamani na kusema yapo makampuni mengine ni makubwa lakini hawezi kuyataja kwa majina na kusema watu watajua pindi wakishafikishwa mahakamani.
"Mkoani Arusha tunamalalamiko mengi ya wanachama na wafanyakazi kwamba michango yao hailetwi kwa wakati au ikiletwa haisomi sasa imebidi tuchukue hatua kwa wakati ambazo ni makini, kuna waajiri wakubwa, wakati na wadogo lakini kwenye mkoa wetu kuna waajiri kama 126 ambao ni sugu hawatimizi wajibu wao kuleta michango ya wafanyakazi wao, waajiri wote tumeshawapelekea onyo la mwisho ratiba inayobakia ni kuwapeleka mahakamani, hivyo hatuna haja ya kuwataja sasa sababu wiki ijayo kesi inaanza mamahakani" alisema Frank Magu
Aidha Meneja Kiongozi wa Shirika la Hifadhi ya Jamii mkoani Arusha amesema kuwa makampuni yote hayo yamefunguliwa shtaka la kukatisha michango ya wanachama wa NSSF na kusema kitendo cha waajiri kutolipa michango hiyo kunapelekea wafanyakazi wao kushindwa kutibiwa, huku wengine wakishindwa kupata mafao ya uzazi kwa kuwa waajiri wanakuwa hawapeleki michango ya wafanyakazi wao.