Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga ameingia matatani baada ya wabunge wa Jubilee kutaka ang’oke kwenye nafasi hiyo ikiwa siku chache baada ya jaji huyo kutengua matokeo ya urais yaliyompa ushindi mgombea Uhuru Kenyatta.
Mbunge wa Nyeri Mjini kwa tiketi ya Jubilee, Ngunjiri Wambugu amefungua mashtaka katika Tume ya Majaji akitaka Jaji Maraga ang’olewe kwa kile alichokieleza kuwa ‘utendaji wake mbaya’.
Mbunge huyo aliyewasilisha mashtaka yenye kurasa 14 ameomba Tume ya Majaji kwa kushirikiana majaji na mahakimu kuanzisha uchunguzi dhidi ya Jaji Maraga ili kubaini mwenendo wake tangu alipoteuliwa kwenye wadhifa huo.
Wambugu anadai kuwa Jaji Maraga ametekwa na kundi la mashirika ya kiraia ambayo yamekuwa yakiendesha kampeni dhidi ya urais wa Kenyatta tangu mwaka 2013.
Pia, anadai jaji huyo alimzuia Jaji Mohamed Ibrahim kushiriki katika kesi iliyofunguliwa na mgombea wa Nasa, Raila Odinga aliyekuwa akipinga matokeo ya urais. Jaji Ibrahim alikatiza siku ya pili kusikiliza kesi hiyo kutokana na kuugua.