Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli anawasubiri wabunge watatu kujibu maswali kwa nini majina yao yamekuwa yakitajwa mara kwa mara katika ripoti zinazohusu ufisadi katika nyadhifa walizowahi kusimamia serikalini.
Hatua hiyo inawaweka wabunge hao kwenye wakati mgumu na kuna uwezekano wa kutopitishwa tena kwenye vikao vya juu ndani ya chama hicho katika mchakato wa uchaguzi mkuu 2020, licha ya kukubalika majimboni.
Wabunge hao ni Andrew Chenge (Bariadi), William Ngeleja (Sengerema) na Profesa Sospeter Muhongo (Musoma Vijijini).
Wabunge hao walitajwa katika sakata la Tegeta Escrow kwa tuhuma tofauti huku Chenge akionekana tena katika sakata la ununuzi wa rada alikolazimika kujiuzulu uwaziri wa Miundombinu katika serikali ya awamu ya nne iliyoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Kwa upande wao, Ngeleja na Profesa Muhongo wametajwa pia katika sakata la makinikia ya madini kupitia nafasi zao kama mawaziri wa zamani wa Nishati na Madini. Hatua hiyo iko mbioni kuchukuliwa kama utekelezaji wa ahadi ya mwenyekiti huyo wa CCM.
Akizungumza wakati wa kukabidhi ripoti ya Tanzanite na almasi, Spika wa Bunge, Job Ndugai alionyesha kusikitishwa na wanasiasa hasa wabunge ambao wamekuwa wakitajwa katika ripoti nyingi za ufisadi, lakini bado wanarejea bungeni kwa kuchaguliwa.
Alisema pamoja na wabunge hao kutajwa kwenye matukio ya namna hiyo wakirudi majimboni wanachaguliwa na wananchi kwa kuwa wao hawajui tabia zao.
“Vyama vya siasa vinawapitisha, wanashinda ubunge na wakija mimi nitawaapisha na juzi Profesa Lipumba (Ibrahim) kaniletea wapya nimewaapisha,” alieleza Ndugai.
Baada ya kauli hiyo, Rais Magufuli alisema ni kweli kuna watu wametajwa kwenye ripoti nyingi na wakiwa bungeni wamekuwa wakichangia hoja kwa nguvu zote. Rais Magufuli alimuuliza Ndugai kama bungeni hawana utaratibu wa kuwashughulikia watu wa namna hiyo au hata kubadili kanuni ili waweze kushughulikiwa.
Hata hivyo, alisema kwa kuwa yeye ni mwenyekiti wa CCM anasubiri barua ya Spika na ikiwafikia watawashughulikia kwa mujibu wa miiko ya chama huku akiamini na vyama vingine navyo vitafanya hivyo.
Hoja ya kuwabana wanasiasa wenye tuhuma za ufisadi ziliibuka baada ya wanasiasa wengi hasa wabunge kutajwa kwenye ripoti mbalimbali zilizochunguza tuhuma za ufisadi. Wabunge wa CCM waliotajwa katika ripoti hizo na ambao hawana nafasi serikalini kwa sasa ni Ngeleja, Profesa Muhongo na Chenge. Wakati wa kashfa ya Escrow, Ngeleja, Chenge na Victor Mwambalaswa (Lupa-CCM) walilazimika kujiuzulu uenyekiti wa kamati mbalimbali za Bunge baada ya kutuhumiwa kupokea mgawo wa fedha za Escrow.
Ngeleja alidaiwa kupokea Sh40.4 milioni, Chenge Sh1.6 bilioni na Mwambalaswa alidaiwa kuwa na mgongano wa kimaslahi. Mbunge mwingine ni Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini) aliyedaiwa pia kupokea Sh1.6 bilioni katika mgawo wa Escrow na kulazimika kujiuzulu uwaziri wa Nyumba na Maendeleo na Makazi.
Kuhusu Chenge
Chenge alitajwa katika kashfa ya ununuzi wa rada ambayo ilimlazimu kuachia uwaziri. Rada hiyo ilinunuliwa kutoka kampuni ya BAE System ya Uingereza kwa Dola40 milioni mwaka 2001, kiwango kilicholishtua hadi Bunge la Uingereza.
Katika uchunguzi wa suala hilo kupitia Serious Fraud Office (SFO), ilibainika kuwa Chenge aliyekuwa mwanasheria mkuu wakati biashara hiyo ikifanyika alikuwa na akaunti kwenye kisiwa cha Jersey iliyokuwa na zaidi ya Dola1 milioni (sawa na zaidi ya Sh1.8 bilioni kwa kiwango cha sasa).
Katikati ya kashfa ya sakata hilo, Chenge aliyekuwa ziarani China akiwa na Rais Kikwete aliporejea aliwaambia waandishi waliomzonga kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuwa fedha hizo ni “vijisenti”. Hata hivyo, baadaye aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kujitetea kuwa ni mwadilifu, mtu safi na hakutenda kosa katika kashfa hiyo.
Pili, Chenge alitajwa kwenye sakata la Escrow akidaiwa kupokea Sh1.6 bilioni kutoka kwa wamiliki wa IPTL.
Akizungumzia kashfa hiyo, mbunge huyo aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti alisema kwa kilugha kuwa yeye ni ‘nyoka wa makengeza’.
Mbali ya kuwa waziri wa Miundombinu kati ya 2006-2008, pia aliongoza Wizara yaa Ushirikiano wa Afrika Mashariki mwaka 2006.
Pia Chenge aliwahi kupewa jukumu la kuongoza Kamati ya Maandishi ya Bunge Maalumu la Katiba iliyoandaa Katiba Inayopendekezwa.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee alijaribu kumtaja waziwazi kuwa anahusika katika mikataba yenye matatizo, lakini mwanasheria huyo wa zamani alimzima kwa kuomba mwongozo na kumtaka Spika amlazimishe awasilishe ushahidi wa anachokisema, la sivyo aache kuchafua watu.
Wabunge Watatu Uso kwa Uso na Magufuli Kutoa Mjibu ya Kutajwa Katika Ripoti za Ufisadi
0
September 13, 2017
Tags