Naibu waziri wa elimu, sayansi na teknolojia amevitaka vyombo vya usalama, jeshi la Polisi na TAKUKURU kufanya uchunguzi mara moja na kuwachukulia hatua watumishi wote wa VETA makao makuu waliohusika na ununuzi wa mashine mbalimbali zilizonunuliwa na kusambazwa katika vyuo vya VETA na kushindwa kufanya kazi tangu mwaka 2010.
Mhandisi Manyanya ametoa agizo hilo mara baada ya kutembelea karakana ya chuo cha VETA Mpanda na kuhoji juu ya vifaa na mashine mbalimbali kutofungwa na nyingine kutokamilika ambazo zilinunuliwa kwa mkopo wa benki ya maendeleo Afrika (ADP) kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.6
Mkuu wa chuo cha VETA Mpanda Joshua Matagane amesema kufuatia kushindwa kufanya kazi kwa mashine hizo zilizosambazwa na kampuni ya Cromwell ltd kutoka nchni uingereza mwaka 2010/11 chini ya mkataba namba ADB/05/2008 wamekuwa wakifanya ufuatiliaji wa mashine hizo kwa karibu lakini hawajapata majibu ya kuridhisha.
Mkuu wa wilaya ya Mlele Bi. Rachel Kasanda ambaye amekaimu wilaya ya Mpanda amesema kukosekana kwa mashine hizo kunawanyima haki wanafunzi wa chuo hicho hasa katika kufanya mafunzo kwa vitendo.