Watu wasiojulikana waliovunja ofisi za mawakili za Prime Attorneys wameiba Sh3.7 milioni na nyaraka kadhaa, zikiwemo hati za viwanja.
Msemaji wa ofisi hiyo, wakili Asia Charli amesema licha ya jengo hilo kuwa na ofisi mbalimbali, maduka, saluni na gym ni ya kwao iliyopo ghorofa ya tatu ndiko kumeibwa nyaraka na fedha.
"Kuna nyaraka mbalimbali za wateja na zetu zimechukuliwa na ni za muhimu sana," amesema.
Charli amesema nyaraka kuhusu kesi za mfanyabiashara Yusuf Manji anayewakilishwa na kampuni hiyo zimesalimika.
Mmiliki wa saluni ya Posh Unisex, Fatma Ebrahim amesema wavamizi wasiojulikana wamevunja mlango wa saluni wenye thamani ya Sh2.5 milioni na hakuna mali yoyote iliyoibwa.
Ofisi ya mawakili ya Prime Attorneys imevamiwa usiku wa manane kuamkia leo Jumanne.
Wakili katika ofisi hiyo, Hudson Ndusyepo ambaye ni miongoni mwa mawakili wanaomtetea mfanyabiashara maarufu Manji katika kesi ya uhujumu uchumi, amesema kabla ya wizi huo, waliohusika walimfunga mlinzi kwa kamba.
Ofisi za kampuni hiyo zipo jengo la Prime House lililopo Mtaa wa Tambaza, Upanga jijini Dar es Salaam jirani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Ilala.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni amethibitisha tukio hilo akisema limetokea kati ya saa nane na saa tisa usiku wa kuamkia leo na uchunguzi unaendelea.