Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametangaza vita mpya ya kupambana na watu wanaojihusisha na kuuza dawa zisizosajiliwa na mamlaka husika na kusema hicho wanachokifanya wanavunja sheria za nchi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy ametoa kauli hiyo leo Bungeni wakati akijibu swali la pili la mbunge wa Konde, Khatibu Saidi Haji (CUF) na kuwataka waganga wakuu kushiriki kikamilifu katika zoezi la kukabiliana na wanaouza dawa zisizosajiliwa na baraza pamoja na TFDA wachukuliwe hatua stahiki.
"Tuna sheria ya tiba asili na tiba mbadala ya mwaka 2002 na kanuni zake, kwa mujibu wa sheria hizo dawa zote za tiba asili au tiba mbadala ni lazima zisajiliwe na baraza la tiba asili na tiba mbadala baada ya kuwa zimethibitishwa na Mkemia Mkuu wa serikali pamoja na TFDA kwamba hazina madhara", amesema Ummy.
Pamoja na hayo, Waziri Ummy ameendelea kwa kusema "tamko langu kwa nchi, yeyote anayeuza dawa za tiba asili zisizosajiliwa anavunja sheria hivyo tutamkamata na kumchukulia hatua ikiwemo dawa za kuongeza nguvu za kiume" amesisitiza Ummy.