Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameelezea maana ya watu wasiojulikana, akisema ni wanaofanya uhalifu na kutoweka bila ya kufahamika.
Hata hivyo, amesema mkakati wa Serikali ni kutaka wajulikane.
Mwigulu amesema hayo leo Alhamisi katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na Kituo cha Redio cha Clouds FM.
Amesema katika matukio kadhaa yaliyofanywa na watu hao, polisi ilipowakamata na kuchunguza ilibaini wawili kati yao walikuwa raia wa kigeni na wengine ni Watanzania.
“Hatujui watu wasiojulikana wanapanga nini, ila nawahakikishia Watanzania kuhusu usalama wao. Tutapambana na mhalifu wa aina yoyote na tutachukua hatua mara moja bila kusita,” amesema.
Amesema mbali ya matukio ya watu wasiojulikana kufanya mauaji Mkuranga, Kibiti na Rufiji, aina ya watu hao ndio wamehusika katika kumshambulia na kumjeruhi kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Amesema polisi wanaendelea kuchunguza kila taarifa inayohusu mazingira ya tukio hilo lililotokea Septemba 7 ijapokuwa kwa sasa asingependa kuzungumzia hatua iliyofikiwa ili kutoharibu upelelezi.
Waziri wa Mambo ya Ndani Mwigulu Nchemba Atoa Maana ya Watu Wasiojulikana
0
September 28, 2017
Tags