Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kinaheshimu maamuzi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Kampeni na Uchaguzi wa chama chao, Samson Mwigamba aliyeandika barua ya kujiuzulu nyadhifa zote za uongozi ndani ya chama hicho.
Akijibu swali wakati akizungumza na wanahabari leo Jijini Dar es Salaam, Katibu wa Itikadi Mawasiliano na Uenezi wa ACT- Wazalendo, Ado Shaibu, amesema kuwa kujiuzulu kwa Mwigamba ni utashi wake na wao kama chama wamekubaliana na uamuzi wake chama kinaheshimu maamuzi yake na si kumshinikiza na kinatambua kwamba Mwigamba bado ni mwanachama wa ACT-Wazalendo.
Akizungumzia tetesi za kuwa ACT-Wazalendo kipo karibu na CCM, Mwigamba amekanusha uvumi huo akisema kuwa chama chao wamekuwa wakali kuikosoa serikali kuliko chama kingine cha siasa.
“Tunaishi katika zama ambazo serikali ya CCM haioni aibu kukandamiza misingi ya haki ya raia na demokrasia. CCM wanaona, upinzani wanaona na kila mwananchi mwenye uelewa anaona.
“Tunaishi katika zama ambazo watu hawaogopi kukandamiza uhuru wa vyama vya siasa na tukiwaachia, wanaweza kulala wakaamuka wamefuta vyama vya siasa. Ukiikosoa serikali kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii unakamatwa,” alisema Shaibu.