Ajibu: Sina Mpango wa Kuwekwa Kwenye Orodha ya Wanaowania Tuzo za Mfungaji Bora

Ajibu: Sina Mpango wa Kuwekwa Kwenye Orodha ya Wanaowania Tuzo za Mfungaji Bora
MSHAMBULIAJI tegemeo wa Yanga, Ibrahim Ajibu ametoa kauli ambayo inaweza kutafsiriwa kuwa ni kama ‘anamzuga’ mpachika mabao wa Simba, Emmanuel Okwi.

Ajibu amedai kuwa yeye hana mpango wa kuwemo katika orodha ya wachezaji wanaowania Tuzo ya Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu huu.

Mpachika mabao wa Simba, Emmanuel Okwi.
Kauli hiyo, imetolewa na Ajibu muda mfupi baada ya kuifungia timu yake bao kisha kumpa asisti Mzambia, Obrey Chirwa katika mchezo wa ligi hiyo dhidi ya Kagera Sugar, Jumamosi iliyopita.

Mshambuliaji huyo al­itua kuichezea Yanga kwenye msimu huu wa ligi kuu akitokea Simba kwa dau la shilingi milioni 50 mara baada ya mkataba wake wa miaka mitatu kumalizika.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Ajibu alisema yeye anachokiangalia hivi sasa ni kuifungia timu yake mabao ili wapate pointi tatu kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya ubingwa.

Ajibu alisema, pointi tatu ndi­yo muhimu ambazo ameahidi kuendelea kufunga na kutengeneza nafasi za mabao kwa wachezaji wenzake ili wafani­kishe malengo yao kama timu waliyoji­wekea.

Aliongeza kuwa, yeye ataendelea kufunga mabao kama kawaida lakini kama ikitokea mwishoni mwa msimu ligi kuu ikamalizika na yeye akawa mfungaji bora, basi atashukuru kwani haikuwa mipango.

“Niseme kuwa, mimi sifungi mabao ili niwe mfungaji, lakini ninafunga mabao ili niiwezeshe timu yangu ushindi na mwisho wa mechi tuchukue pointi tatu.

“Kwani nimesikia tetesi kuwa ninafunga mabao kwa ajili ya kushindana na mchezaji flani (Okwi), hapana mimi ninafunga kwa ajili ya kuiwezesha timu yangu kutwaa ubingwa wa ligi kuu.
“Mimi bado nina deni kubwa na Yanga ambalo bado sijalilipa kama unavyokumbuka wakati ninasajiliwa kuja Yanga nilitoa ahadi kadhaa ikiwemo hii ya ubingwa wa ligi kuu, hivyo ni lazima niitimize.

“Hivyo, nitaendelea kufunga na kutengen­eza nafasi za kufunga mabao kama kawaida na kama ikaja kutokea mwishoni mwa msimu ninakuwa mfungaji bora, basi nitashukuru Mungu kwani haikuwa mipan­go sana,” alisema Ajibu.

Okwi, anaongoza kwenye ufungaji akiwa amefunga ma­bao 7 akifuatiwa na Mohamed Rashid wa Prisons (4), Habib Haji wa Mbao FC, Shiza Kichuya (Simba), Eliud Ambokile (Mbeya City) na Ajibu wote (3).
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad