Ally Hapi Apigania Vikoba Endelevu kwa Walimu

Ally Hapi Apigania Vikoba Endelevu kwa Walimu
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi ameuomba uongozi wa Vicoba endelevu nchini kutanua mtandao ili uweze kuwafikia wananchi wengi zaidi wakiwamo walimu pamoja na wafanyabiashara ndogondogo.

Alisema ikiwa hayo yatafanyika itasaidia kuhakikisha Serikali inafikisha lengo lake la kuyakomboa makundi hayo kiuchumi.

Hapi alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati akizindua taasisi ya Buta-Vicoba Endelevu iliyopo Bunju.

“Niwaombe sana viongozi wa Vicoba mtanue zaidi mtandao wenu ili muwafikie maelfu zaidi ya wafanyabiashara ndogondogo, wafanyakazi mbalimbali wa Serikali wakiwamo walimu na mshirikiane nao katika kuangalia namna bora zaidi ya wao kupata huduma za kifedha ikiwamo mikopo ili waongeze thamani ya mitaji yao,’’ alisisitiza.

Akitoa taarifa ya hali ya vicoba nchini, rais wa Vicoba Endelevu, Devotha Likokola alisema mtandao huo unahusisha vikundi zaidi ya 100,000 vikiwa na wanachama zaidi ya 2,200,000 huku wakiwa na akiba ya zaidi ya Sh1 trilioni.

“Nitoe wito kwa wanajamii wazidi kushiriki katika Vicoba Endelevu kwa kuwa ni mfumo ambao tayari umeonyesha kuwa unaweza kuwaondoa katika umaskini,” alisema.

Akizungumza katika uzinduzi huo, mkurugenzi wa Buta-Vicoba Endelevu, Semeni Gama alisema taasisi hiyo inahusisha vikundi 128 kutoka mikoa mbalimbali ikiwamo Mbeya, Kigoma, Lindi, Tanga na Njombe ikiwa na wanachama 2,186.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad