CCM Monduli, Shinyanga Wapata Viongozi Wapya

CCM Monduli, Shinyanga Wapata Viongozi Wapya
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Monduli kimemchagua Wilson Lengima Kurambee kuwa mwenyekiti wa chama hicho wilaya baada ya kupata kura 429 akiwaacha mbali washindani wake Amani Silanga Mollel(78) na Hamisi Ramadhani Puzza(9).

Katibu wa CCM wilaya ya Monduli, Gurisha Mfanga ameliambia Mwananchi kuwa uchaguzi huo ulifanyika kwa amani kwa kuzingatia kanuni za chama hicho za kuwapata viongozi wake hatua inayokifanya kuwa chama cha kupigiwa mfano barani Afrika.

Mfanga alisema nafasi ya Katibu Mwenezi wa Wilaya ilinyakuliwa na Lorinyu Mkoosi baada ya kupata kura 68,Jeremia Laizer kura 11 na Sakaya Kabuti hakupata kitu huku waliochaguliwa kuwa wajumbe wa mkutano mkuu taifa ni Paulo Oljumbe Kiteleki aliyepata kura 364, Hussein Ally Warisama (292) na Magdalena Richard Mhina (235).

“Uchaguzi umefanyika kwa amani na utulivu, kipekee ninawashukuru wapigakura na mkuu wetu wa wilaya, Idd Kimanta kwa ushirikiano mkubwa aliouonyesha katika zoezi zima hii inamaanisha Monduli imezaliwa upya na hakuna tena kupangiwa viongozi kama zamani,”alisema Mfanga

Alisema uchaguzi huo unatoa ishara njema ya chama chake kufanya vizuri kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Moita Novemba 26 mwaka huu ambayo diwani wake kupitia Chadema, Edward Sapunyo alijiuzulu na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Wakati Monduli wakipata viongozi hao Kanali Tajiri Maulidi aliyekuwa anatetea kiti chake cha uenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ameangukia pua kwa kupata kura 162 dhidi ya mpinzani wake Abubakar Gulam aliyepata kura 246.

Hata hivyo, licha ya Maulid kusema kwamba hana kinyongo na mshindi huyo lakini alisema “zipo kasoro katika chaguzi nawaomba wasimamizi lazima waondoe kasoro hizo, kama vile kura zikizidi lazima mtu alalamike,” alisema bila kufafanua huku akiahidi kutoa ushirikiano

Katika uchaguzi huo wapiga kura walikuwa 408.

Kwa upande wake aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi Jumnne Kitundu ambaye ni katibu wa CCM wilaya ya Shinyanga aliwataka viongozi hao wasitumie maneno makali ya kuwakashifu wenzake pia aliwataka viongozi wawe na mshikamano ili chama kiweze kusonga mbele.

Awali Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Haula Kachwampa aliwataka viongozi wote waliochaguliwa katika uongozi wawe na upendo kwa kufuata misingi ya chama.

Hayo ameyasema jana kwenye uchaguzi wa mwenyekiti na wajumbe CCM wilaya ya Shinyanga mjini uliofanyika katika ukumbi wa CCM Kambarage.

“Kwa kweli mimi binafsi sijapendezwa na hali ya kuchafuana kwani asili ya chama chetu ni kupendana na kudumisha upendo hivyo tunaomba mtuamini majina tuliyowaletea chama kimejiridhisha,” alisema Kachwampa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad