Chama cha CCK Chajiandaa Kufanya Mkutano Ikulu

Chama cha CCK Chajiandaa Kufanya Mkutano Ikulu
Chama cha Kijamii (CCK) kinajiandaa kufanya mkutano wake mkuu mapema mwakani katika ofisi ya Rais, Ikulu ya Dar es Salaam.

Mpango huo umetangazwa na mwenyekiti wa chama hicho, Constantine Akitanda ikiwa ni siku chache baada ya Rais John Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM kuvialika vyama vya upinzani kufanya mikutano yake Ikulu kama chama hicho kinavyofanya baadhi ya mikutano yake.

Kauli ya Rais Magufuli ilikuja huku kukiwa na malalamiko ya baadhi ya vyama vya siasa ikiwemo Chadema vikisema CCM imekiuka Sheria ya Vyama vya Siasa inayokataza vyama vya siasa kutumia rasilimali za Serikali kwa manufaa yake.

Akifungua mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kilichofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Rais Magufuli alisema:

“Nawakaribisha sana hapa Ikulu hapa ni kwenu. Bila ninyi mimi nisingekuwa hapa. Kwahiyo sioni aibu kuwakaribisha wana CCM, lakini pia hapa ni kwa Watanzania wote, na ndio maana kuna wageni kutoka nje wamefika hapa Ikulu, wanamuziki niliwakaribisha Ikulu, wakati wa futari tulifanyia hapa hapa.

“Kwahiyo sioni ajabu ninyi kuwakaribisha hapa. Halafu kuona watu wajiulize kwanini mikutano wanafanyia Ikulu,” alisema Rais Magufuli.

Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili leo Jumanne, Mwenyekiti wa CCK, Akitanda amesema wameipokea kauli hiyo ya Rais na wataitekeleza kwa kufanya mkutano wao mkuu mapema mwakani.

Amesema awali walipanga kufanyia kikao cha Kamati Kuu Ikulu, lakini wameona wasogeze mbele ili wafanye mkutano mkuu Februari mwakani.

“Tunataka kutumia ukumbi wa Ikulu kama alivyoelekeza Rais, maana ni ukumbi wa wananchi wote,” amesema Akitanda.

Aliongeza: “Tulitaka tuombe ukumbi wa Ikulu kwa ajili kikao cha Kamati Kuu wiki ijayo, lakini tukaona kikao hicho kitakuwa na wajumbe wachache tu yaani 30, sasa tunajipanga kufanya mkutano mkuu utakaokuwa na wajumbe 500 maana ule ukumbi ni mkubwa sana.”

Ameongeza pia sababu za kusogeza mbele mkutano wao ni barua waliyopokea kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ikiwataka wauandae mkutano huo kwa miezi minne.

“Chama kimepokea barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo inatuelekeza kufanya maandalizi ya Mkutano Mkuu ndani ya miezi minne, nadhani kuanzia mwezi huu itakuwa Februari mwakani,” amesema Akitanda.

“Katiba yetu inasema Mkutano Mkuu utakuwa na wajumbe 500, lakini hata wakiwepo nusu yake wanaweza kufanya uamuzi. Tunaamini kabisa Rais atatukubalia kufanyia mkutano Ikulu, akikataa basi tutajua kwamba hatufai, lakini hatutarajii kukataliwa,” ameongeza.

Amesema kabla ya mkutano huo, kutakuwa na vikao vya utangulizi vitatu ambavyo ni pamoja na kamati ya utendaji, sekretarieti na mwisho Kamati Kuu ambayo itapendekeza tarehe ya Mkutano Mkuu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad