Chama Cha Wananchi (CUF) kimetoa pongezi kwa Sheikh Ponda baada ya jana kuwataka Watanzania bila kujali itikadi zao na imani zao za dini kwa pamoja kushikamana kutetea na kulindwa kwa haki za binadamu, uhuru wa Kidemokrasia na utawala wa sheria.
Sheikh Ponda alisema hayo jana baada ya kumtembelea Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu jijini Nairobi anakopatiwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi mnamo Septemba 7, 2017 mjini Dodoma.
Kufuatia kauli hiyo wa Sheikh Ponda Chama Cha Wananchi CUF kimempa pongezi kiongozi huyo kwa uthubutu wake wa kusema ukweli na kukemea maovu mbalimbali ambayo yanaendelea nchini.
"Tunampongeza kwa kujitokeza katika kipindi hiki ambacho Watanzania na Viongozi wengi wa dini na kisiasa wamejazwa woga, wale waliokuwa mstari wa mbele kukemea maovu katika awamu zilizopita hivi sasa wamejitia upofu, ububu na uziwi. Tunampongeza kuelezea Umuhimu na Ulazima kwa Watanzania kuungana pamoja kutetea uwepo wa mfumo wa Haki, Demokrasia na Utawala wa Sheria kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" alisema Mbarala Maharagande
Aidha Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa CUF, Mbarala Mharagande amedai kuwa wao CUF wanatarajia viogozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wasomi mbalimbali, waandishi wa Habari na wananchi kwa ujumla hawapaswi kukaa kimya bali wanapaswa kukemea mambo mabaya ambayo yanaendelea nchini, huku wakivitaka vyombo vya dola kutekeleza wajibu wao.