CUF Wagoma Maalim Seif Kupimwa Akili

CUF Wagoma Maalim Seif Kupimwa Akili
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi, Ahmed Nassor Mazrui amesema Katibu Mkuu wa CUF hatopimwa akili na wale wanaosema Maalim Seif Shariff Hamadi akafanyiwe uchunguzi huo ni vyema wakaenda wao.

Mazrui alisema Maalim Seif hawezi kupimwa akili kwa kuwa yupo ngangari na ana akili timamu kwa kila anachokifanya; kwa maslahi ya chama na Wazanzibari kwa ujumla.

Akizungumza katika mkutano mkuu wa wilaya ya Mjini wa chama hicho hapa Zanzibar juzi, Mazrui alisema Maalim Seif ni mwenye akili timamu na kutaka wote wanaotoa madai hayo ya kupima akili wapuuzwe.

Alisema kuonyesha katibu huyo ni mwenye akili timamu amekuwa akigombea nafasi ya urais ndani ya chama hicho kwa kipindi cha miaka 25 bila ya kuchoka, kutetereka wala kukata tamaa.

Alisema katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Maalim Seif ndiyo nguli wa siasa na kuwataka wafuasi wa chama hicho kutovunjika moyo kwani kiongozi wao huyo yupo makini na anaendelea kuidai haki ya Wazanzibari "iliyoporwa" Oktoba 25, 2015.

Matokeo ya awali ya urais wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa 2015 yalionyesha Maalim Seif alikuwa akiongoza katika kinyang'anyiro hicho ambacho waangalizi wa kimataifa, ikiwemo Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Ulaya na Marekani, walidai kilifanyika kwa haki na amani.

Hata hivyo, uchaguzi huo wa rais na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ulifutwa kwa Tume ya Uchaguzi (ZEC) kwa maelezo kuwa ulikuwa na kasoro nyingi za msingi, ikiwemo idadi ya kura katika baadhi ya vituo kuvuka jumla ya wakazi waliojiandikisha.

“Mwenye kusubiri hajutii," alisema Mazrui, "kwa hivyo (wanachama) vuteni subra".

"Mambo yapo, sisi watendaji wakuu tushajiandaa kuchukua serikali.”

Aliwataka wafuasi hao kutoyumba wala kurudi nyuma na badala yake kumuunga mkono Katibu Mkuu ambaye alidai anafanya kazi kubwa ya kudai na kutetea haki ya Wazanzibari.

“Niwaombe wafuasi wa CUF musirudi nyuma, atakayerudi nyuma atakuja kuchujwa kwa chujio na kuachwa nyuma.”

Aidha, Mazrui alisema licha ya migogoro na usaliti mkubwa unaofanywa na baadhi ya watu kwa chama hicho, bado CUF haijatetereka na ipo imara.

Alisema CUF inaendelea na vikao vyake kama kawaida na chama hicho kinasonga mbele licha ya kuwa hakina ruzuku kwa sasa.

Alisema chama hicho kinaendelea kupambana kwa kutumia njia sahihi bila ya kuwaangamiza wanachama wake kwani viongozi wa CUF wanafanya kila njia kusimamia haki na kudai mamlaka kamili ya Zanzibar.

Aidha, aliwataka wafuasi wa chama hicho kukosoana ndani ya vikao vya chama badala ya kusemana nje.

Tags

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Hilo jina la "MAZRUI" linaniikumbusha mbali saana. Enzi za Tip Tippu na waarabu wa Mazrui.

    ReplyDelete
  2. Ndivyo ilivyo....
    Ulisha pata kusikia WITU?

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad