Pambano la wikiendi hii kati ya vinara wa Kundi C, Dodoma FC utaamua hatma ya Toto Africans kuweka hai au kuzika matumaini yake ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao.
Timu hizo zitakutana Jumamosi, huku Dodoma ikiongoza kundi na alama 15 wakati Toto Africans ipo nafasi ya saba ikiwa na pointi tano tu baada ya kila timu kucheza mechi saba.
Iwapo Dodoma itaibuka na ushindi kwenye mechi hiyo itafikisha pointi 18 na hivyo kuhitaji ushindi katika mechi tatu tu za duru la pili ili Toto isiweze kuifikia.
Na kama ikitokea Alliance inayoshika nafasi ya pili ikaibuka na ushindi dhidi ya JKT Oljoro katika mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza, itatakiwa kupata ushindi katika mechi zake nne kati ya saba za mzunguko wa pili ili kuinyima rasmi Toto nafasi mbili za kupanda Ligi Kuu msimu ujao.
Kama Dodoma FC itaifunga Toto na kisha kupata ushindi katika mechi tatu zijazo itakuwa na pointi 27, wakati Alliance ikiifunga Oljoro na kupata ushindi kwenye mechi nne zitakazofuata, itafikisha pointi 28 ambazo hazitoweza kufikiwa na Toto Africans hata kama itapata ushindi kwenye mechi zote saba za mzunguko wa pili.
"Pasi na shaka, mechi yetu dhidi ya Dodoma FC ndio nafasi ya mwisho kuona kama bado tunaweza kuwa na nafasi ya kupanda au ndio basi tena," alisema Kocha wa Toto, Almas Moshi.
Kocha huyo alidai kikubwa kinachowakwamisha ni hali mbaya ya kifedha ambayo inawafanya wakose maandalizi mazuri kabla ya mechi zao.