Gavana mteule wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amesema amepokea kwa heshima kubwa dhamana aliyopewa na Rais John Magufuli na anatambua changamoto za nafasi hiyo.
Profesa Luoga ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) - Taaluma, amesema leo Jumatatu Oktoba 23,2017 kuwa atatumia wataalamu wa BoT kufanya kazi.
Amesema anahitaji ushirikiano wa kila mtu katika kufanikisha kazi aliyopewa.
“Nimepokea kwa heshima dhamana niliyopewa nikitambua kwamba zipo changamoto. Nitakwenda kujifunza zaidi kwa sababu sijawahi kuwa Gavana, nitatumia wataalamu waliopo katika kutekeleza majukumu yangu,” amesema Profesa Luoga.
Soma: Profesa Luoga Gavana mpya BOT
Rais Magufuli Julai 11,2017 alimteua Profesa Luoga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akichukua nafasi ya Bernard Mchomvu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa Novemba mwaka jana na bodi hiyo kuvunjwa.
Profesa Luoga ni mtaalamu katika masuala ya sheria za kodi na amefundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tangu mwaka 1986 kabla ya kupandishwa cheo na kuwa profesa mshiriki (Associate Professor) mwaka 2005.
Ameshika nafasi mbalimbali chuoni hapo ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wa kamati ya misaada ya kisheria katika kitivo cha sheria mwaka 1993 - 1995, mkurugenzi wa masomo ya shahada za awali (2005 - 2009), katibu wa baraza la chuo kikuu (2009 - 2013) na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma (2013 hadi sasa).
Profesa Luoga aliyezaliwa mwaka 1958 ni wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Alihitimu shahada ya kwanza ya sheria UDSM mwaka 1985. Baadaye alikwenda kusoma Shahada ya Uzamili (LLM) katika chuo cha Queen’s University cha Canada (1988).
Mwaka 1988 alihitimu Shahada ya Uzamili ya Sheria za Kimataifa (MIL) katika Chuo cha Lund University cha Sweden (1991) na Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Warwick cha Uingereza mwaka 2003.