Hivi Ndivyo Mwalimu Nyerere Anavyokumbukwa Na Watanzania

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anaweza kuwa aliondoka duniani mwaka 1999, lakini miaka 18 baada ya kifo chake anaendelea kuishi; hotuba zake zimejaa katika mitandao.

Mwalimu Nyerere, ambaye aliliongoza Taifa la Tanganyika kupata uhuru mwaka 1961 na baadaye kuliunganisha na Zanzibar mwaka 1964, alifariki akiwa London, Uingereza ambako alikwenda kutibiwa.

Aliliongoza Taifa la Tanzania kwa takriban miaka 24 chini ya siasa za chama kimoja, lakini baada ya kung’atuka mwaka 1985 alikuwa mtetezi mkubwa wa demokrasia na hasa suala la kuandika Katiba bora itakayowapa wananchi haki na nguvu ya kudhibiti viongozi wao.

Msimamo huo ndio umemfanya Mwalimu Nyerere aendelee kuishi katika dunia ya leo, kiasi cha vijana ambao hawakuwahi kumuona akiwa hai sasa wanamjua kutokana na video zake kusambazwa kila mara kunapotokea tukio ambalo aliwahi kulizungumzia.

Video za hotuba zake kwenye youtube zinapata watazamaji kuanzia 1,600 hadi takriban 450,000 na nyingi zina urefu wa kati ya dakika 1:58 na dakika 17:51

Lakini zile zinazorushwa katika mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na WhatsApp ni za urefu wa chini ya dakika 1:30.

Katika hotuba nyingi alizowahi kutoa sehemu tofauti, inayosambazwa sana ni ya mikutano yake na waandishi wa habari nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam, ikiwamo aliyozungumzia suala la Muungano na umuhimu wa kuheshimu Katiba na sheria.

Alilazimika kuitisha mkutano huo na waandishi wa habari baada ya kuibuka suala la Zanzibar kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), kinyume na Katiba.

Hotuba nyingine ambayo vipande vyake vinasambazwa kila mara kwenye mitandao ya kijamii ni ile aliyoitoa alipoongea na waandishi wa habari Hoteli ya Kilimanjaro, alipozungumzia sifa za mtu anayefaa kuwa rais na Muungano.

Lakini suala la Katiba ndilo limevutia sana watumiaji wa mitandao ya kijamii.

“Katiba haiwezi kupuuzwa. Akishachaguliwa mtu ataapishwa kuilinda Katiba ili tuweze kumshtaki aliyeikiuka. Mtu yeyote ambaye hawezi kuilinda wala kuisimamia Katiba baada ya kuchaguliwa, hatufai,” anasema katika moja ya hotuba hizo.

“Nchi haiendeshwi kwa matamko wala kwa akili za mtu, bali kwa Katiba itakayowapa wananchi haki ya kufahamu nini kitatokea kesho kwa kuwa hiyo ni haki yao.”

Vipande vya video vya nukuu hizo vimekuwa vikirushwa mara kwa mara kwenye mitandao ya kijamii kila wakati suala la Katiba mpya linapoibuka.

Na wakati wanasiasa wa upinzani walipoibuka na hoja ya kutaka waendeshe maandamano nchi nzima kupinga kile wanachokiita udikteta katika operesheni waliyoita Ukuta, watumiaji wa mitandao hiyo nao walikuwa na nukuu ya Mwalimu Nyerere inayoeleza maana ya neno hilo.

“Udikteta ni serikali ya mtu mmoja au kikundi cha watu wachache. Na wao ndiyo huwa sheria. Anayepinga watakayo, basi huonyeshwa cha mtemakuni,” anasema Mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba hizo.“Tuzungumze. Mambo ya nchi yazungumzwe waziwazi katika vikao rasmi vilivyowekwa. Nchi yetu inaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na maamuzi makubwa ya nchi yanatokana na vikao na bungeni walivyotaka janja janja ya kuyatoa, hizi ndizo dalili za dictatorship. Lazima zikemewe pamoja na janja janja.

Wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, watumiaji wa mitandao walikuwa na ujumbe kutoka kwa Mwalimu Nyerere.

Katika video hiyo, Mwalimu Nyerere anazungumzia umuhimu wa chama kuzingatia maoni ya wengi wakati wanapoteua mgombea urais wa CCM, akionya kuwa wakipuuza mambo yanaweza kutowanyookea.

Video hiyo ilisambazwa baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM.

Akizungumzia hali hiyo ya kuendelea kuishi kwa Baba wa Taifa, mratibu wa tathimini na ufuatiliaji wa Baraza la Maaskofu (TEC) Paul Chilewa alisema inatokana na watu kuona mawazo yake hayafanyiwi kazi.

“Changamoto iliyopo sasa ni kwamba watu wanasikiliza hotuba zake, lakini hawazifanyii kazi. Wanabaki kuzisifia kwa maneno, tofauti na inavyotakiwa,” alisema Chilewa.

“Tunapaswa kusifia hotuba hizo kwa kuleta matokeo chanya. Tujiulize tumepotea wapi? Je kweli nchi inajengwa kwa maendeleo ya wengi au inanufaisha wachache?” alihoji.

Naye Profesa Malise Kaisi alisema Mwalimu Nyerere alikuwa na uwezo wa kuona mbele.

“Aliona umuhimu wa kuwa na siasa ya ujamaa na kujitegemea akisisitiza maendeleo kwa watu na si vitu. Lakini kwa sasa kumekuwa na tofauti kwani maendeleo ya vitu ndiyo yanapewa kipaumbele,” alisema Profesa Kaisi.

Alisema ujenzi wa madaraja ya ghorofa (flyovers) au viwanja vikubwa vya ndege katika kila mkoa, hausaidii kama bado huduma muhimu kwa wananchi zitakuwa zinasuasua.

Naye Sheikh Khamisi Mataka, ambaye ni msemaji wa Mufti, alisema: “Kuzungumzia maendeleo ya watu ina maanisha waweze kupata vitu muhimu, elimu bora , chakula na mavazi na afya bora.” alisema .

“Ili uendelee mbele kwa hatua ni vyema uijue jana yako ilikuwaje je ulijikwaa wapi, ili uweze kuitengeneza leo yako uweze kuipata kesho yako nzuri, wapo wanaosikiliza na kufanyia kazi.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad