Hivi Ndivyo Rais Magufuli Alivyojibu Hoja za Zitto Bila ya Kumtaja
0
October 24, 2017
Kwa takriban miezi miwili, kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amekuwa akihoji ukimya wa Serikali katika kutangaza mapato na hata ilipotangaza, alisema takwimu zimepikwa, lakini jana alipata majibu ya hoja zake.
Rais John Magufuli alitumia hafla ya kutunuku wajumbe wa kamati mbili alizoziunda kuchunguza biashara na udhibiti wa madini, kutoa ufafanuzi kuhusu hali ya makusanyo ya mapato, jambo ambalo Zitto amekuwa akihoji katika mikutano na waandishi wa habari, mikutano ya chama chake na katika mitandao ya kijamii.
Baada ya Benki Kuu (BoT) kutotangaza ripoti ya hali ya kiuchumi kwa miezi miwili kwa kile ilichoeleza kuwa ni ugumu wa upatikanaji wa taarifa, na Mamlaka ya Mapato (TRA) nayo kusuasua kutangaza makusanyo kwa miezi kadhaa, Zitto alisema hali hiyo ilitokana na Serikali kukusanya fedha kidogona kwamba ilikuwa ikipika taarifa.
Katika hotuba yake jana, Rais Magufuli hakumtaja mtu anayepotosha takwimu za Serikali, lakini alihoji hoja anazozitoa na kutaka hatua zichukuliwe.
“Nafikiri kama sikumbuki vizuri, Sheria ya Takwimu ya 2015, kuna kifungu kinasema mtu anayebadilisha takwimu za Serikali anaweza kufungwa miaka miwili jela,” alisema Rais.
“Unakuta mtu anazungumza makusanyo yameshuka, wakati anajua si kweli. Watu wa namna hii wangekuwa wanapelekwa mahakamani waka-justify (wakathibitishe).”
Alisema kwa hesabu za kawaida, kama mapato yanashuka, Serikali haiwezi kusaini mkataba wa kujenga reli yenye thamani ya zaidi ya Sh7 trilioni na urefu wa kilomita zaidi ya 700.
Pia alisema kwa Serikali ambayo haina mapato, haiwezi kununua ndege sita mpya kwa wakati mmoja.
“Wanazinunua kwa kubadilisha kwa dagaa? Au migebuka ya Kigoma?” alihoji Rais.
Pia alisema kwa Serikali ambayo haina fedha, haiwezi kufufua mradi mkubwa wa kuzalisha umeme kama wa Stiegler’s Gorge ambao ukikamilika utakuwa unazalisha megawati 2,100, wakati uwezo wa sasa ni megawati 1,460.
Alisema kutokana na kuwa na fedha, Serikali imetangaza zabuni ya mradi huo na zaidi ya kampuni 79 zimejitokeza kuwania kupata zabuni hiyo.
“Zabuni za mradi huu zimeshatangazwa na fedha zimeshatengwa. Kama mapato yamepungua tungepata wapi fedha,” alihoji Rais Magufuli.
“Kama huna fedha na makusanyo hayapo, utatangaza tenda ya namna hiyo? Utakuja kuwalipa nini?” alihoji Rais.
Akiendelea kufafanua kwa mtindo wa maswali, Rais pia alisema Serikali isingeongeza bajeti ya afya wala kutekeleza mradi wa Umeme Vijijini (Rea), kujenga madaraja, barabara kutoka Kigoma hadi Nyakanazi na ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria kama isingekuwa na fedha.
“Kama fedha hakuna utawawekaje makandarasi wale kwenda kujenga barabara kwa kiwango cha lami?” alihoji.
“Kwa hiyo ninachotaka kusema Watanzania muwapuuze watu wa namna hiyo.”
Zitto, ambaye amewahi kuongoza Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), amekuwa akihoji makusanyo ya Serikali na mwishoni mwa wiki alisema ACT Wazalendo imemtaka aende kuwasilisha ripoti kwenye chama kuonyesha jinsi Serikali inavyopika taarifa kuhusu makusanyo na hali ya kiuchumi.