Maduka ya rejareja ya Nakumatt tawi la Arusha limefungwa kutokana na kudaiwa kodi na mmiliki wa jengo la Tanganyika Farmer's Association (TFA).
Mhasibu Kiongozi wa TFA, Evarist Kauki amesema leo Jumanne Oktoba 24,2017 kuwa, mawasiliano yamefanyika kwa muda mrefu kuwataka Nakumatt kulipa deni la kodi ya pango bila mafanikio.
"Ofisi yetu kuu ndiyo ilikuwa na mawasiliano nao ya mara kwa mara, tumewapa kazi kampuni ya udalali ya First World Investment Brokers kuhakikisha hakuna shughuli zinazofanyika kuanzia leo hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi," amesema Kauki.
Duka hilo lilifunguliwa mwaka 2014 baada ya mpangaji wa mwanzo Shoprite kufunga biashara nchini.
Mfanyakazi wa Nakumatt, Angel Makere amesema kufungwa kwa duka hilo kumewashtua kwa sababu kumetokea ghafla licha ya kuwa biashara iliyumba katika siku za karibuni.
Kufungwa duka hilo kumewaacha wafanyakazi zaidi ya 50 kukosa kazi kwa muda usiojulikana.