Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, (CUF) Julius Mtatiro ambaye yupo nchini Kenya amesema kuwa leo Oktoba 8, 2017 amepata bahati ya kumuona Mbunge Tundu Lissu hospitali na kusema kuwa Lissu ni mtu asiyeogopa na mwenye maono makubwa.
Mtatiro anasema kwa muda ambao ameweza kukaa na Lissu hospitali amemwagiza kuwaambia Watanzania kuwa atarudi akiwa mzima na kuendelea na mapambano maradufu zaidi katika kupigania haki.
"Mtatiro nenda kawaambie kuwa nitarudi nikiwa mzima na tutaendelea na mapambano maradufu zaidi, faraja muhimu nayohitaji kutoka kwa Watanzania hivi sasa ni kuendeleza mapambano ya kudai haki na kupambana na udikteta, tusikubali nchi yetu iharibiwe na kikundi cha watu wanaoogopa kukosolewa" alisema Mtatiro
Aidha Mtatiro anasema kumuona Mbunge Tundu Lissu hospitali ni kitu ambacho kimezidi kumjenga zaidi na kumpa mafunzo makubwa katika maisha ya kila siku na katika siasa
"Mimi binafsi kama Mtatiro, kumuona Lissu kumenijenga zaidi, kumenifundisha kuwa ukipigwa risasi hata 100 kwa sababu ya kuwa mkosoaji wa watawala yapo mambo mawili yatatokea, aidha utapona kama Lissu au utakufa kama ilivyowatokea wapigania haki wengi. Uki-survive kama Lissu jambo moja litatokea, utaungana na wananchi wote kupigania haki kwa nguvu kubwa zaidi. Ukiuawa kwa risasi kama wapigania haki wengi jambo moja kubwa litatokea, kifo chako kitapandikiza mbegu kubwa ya ukombozi, kifo chako kitaliamsha taifa kupigania haki na kupambana na madikteta wajinga" alisisitiza Mtatiro
Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 na kisha baada ya hapo alipelekwa nchini Kenya jijini Nairobi kwa matibabu zaidi ambapo mpaka sasa yuko Kenya kwa matibabu.