Kairuki Amkaidhi Mkuchika Zigo la Vyeti Feki Afunguka Changamoto ya Vyeti Feki Ilivyomtesa

Kairuki Amkaidhi Mkuchika Zigo la Vyeti Feki Aeleza Changamoto ya Vyeti Feki Ilivyomtesa
Waziri wa Madini, Angellah Kairuki amesema uhakiki wa vyeti ni changamoto aliyokumbana nayo alipokuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Amesema hayo leo Jumatano alipokabidhi ofisi kwa Waziri mpya wa Utumishi, George Mkuchika. Amesema changamoto ya uhakiki wa vyeti hawezi kuisahau.

"Nchi kama vile Afrika Kusini, India na Pakistan walifanya jambo kama hili kwa awamu na bado hawajamaliza, lakini sisi tumelifanya kwa jumla, haikuwa kazi nyepesi," amesema.

Kairuki amesema mbali ya uhakiki, baadhi ya watendaji alioshirikiana nao hawakuwa waaminifu ambao walipenyeza watu wasiokuwa na sifa.

"Waliopenya katika hatua hii naamini Mkuchika atapambana nao ipasavyo," amesema Kairuki.

Amesema uhakiki ulichukua muda mrefu kiasi cha kuwakatisha tamaa watumishi wa umma.

Masilahi ya watumishi wa umma amesema lilikuwa changamoto nyingine kwa sababu Serikali inatamani kuyaboresha lakini fedha inayokusanywa haikidhi mahitaji.

Amewatoa shaka watumishi ambao hawajapandishwa madaraja akisema fedha kwa ajili watumishi zaidi ya 163,000 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza hilo.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ofisi, waziri Mkuchika amesema mbali ya  kuendeleza mazuri aliyoyaacha Kairuki, ikiwemo kudumisha nidhamu katika utumishi wa umma, atasisitiza elimu ya kupiga vita rushwa.

Mkuchika amesema atazungumza na Waziri wa Elimu ili elimu ya kupiga vita rushwa ianze kutolewa kuanzia shule ya msingi.

Amesema nchi zilizofanikiwa kupiga vita rushwa ziliwekeza katika kutoa elimu juu ya madhara yake.

"Miaka ya nyuma ilikuwa hakuna mtu mwenye kuheshimika kama mtumishi wa umma. Wasomi wenye weledi na ujuzi walikuwa watumishi wa umma, hapa kati hali ikabadilika,” amesema.

Mkuchika amesema kazi iliyopo ni kuirudisha nidhamu hiyo na kuhakikisha watumishi wa umma wanakuwepo ofisini muda wote kutoa huduma kwa wananchi.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad