Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk Juma Malewa amewaagiza wakuu wa magereza nchini kutumia rasilimali zilizopo kwenye maeneo ya vituo vyao vya kazi ili kukabiliana na changamoto zilizopo, ikiwemo kupunguza uhaba wa nyumba za askari.
Ametoa kauli hiyo baada ya kukagua Gereza la Mkuza lililopo Picha ya Ndege wilayani Kibaha akiwa ziarani kujionea changamoto zilizopo.
Dk Malewa amesema jana Jumatatu kuwa changamoto zilizopo katika gereza hilo ni uchache wa nyumba za askari na zilizopo zimechakaa hivyo kuhitaji ukarabati.
“Nitoe wito kwa askari waweze kutumia rasilimali zilizopo ili kukabiliana na hali hiyo wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kuzitatua," amesema.
Amesema wanaweza kufyatua matofali na kuyachoma na wale ambao kuna miti kwenye maeneo yao wanaweza kutengeneza mbao ili kujenga nyumba za kuishi askari za gharama nafuu.
Kutokana na umuhimu wa askari wa Jeshi hilo, amesema Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuboresha makazi.
Amesema hivi karibuni Rais John Magufuli ametoa fedha zitakazotumika kujenga nyumba za askari zipatazo 300 katika Gereza la Ukonga.
Dk Malewa amesema nyumba zingine tano zitakazokuwa na uwezo wa kuishi askari 60 zinatarajiwa kuzinduliwa mkoani Arusha.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Pwani, Boidy Mwambingu amesema wameshaanza ujenzi wa nyumba mbili za askari katika Gereza la Bagamoyo na pia wanaendelea na ujenzi wa zahanati ya Gereza la Mkuza.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alimuomba Dk Malewa kuangalia uwezekano wa kutenga bajeti ya kutosha na hasa kwa ajili ya kulipia bili za maji na umeme kwenye majengo ya Magereza kuepusha taasisi hiyo muhimu kukatiwa huduma hizo.