Kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole imezua hofu miongoni mwa wabunge wa chama hicho, huku wengi wakisita kutoa maoni yao.
Polepole alinukuliwa na Redio Times juzi akisema kuwa wanachama wa CCM wanaotaka kugombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa 2020 wanatakiwa kuwa wakazi wa eneo husika.
Inakadiriwa kuwa nusu ya wabunge wa CCM hawaishi katika majimbo yao kwani wengi wao wanaishi mijini na hasa Dar es Salaam jambo ambalo linaweza kuwatoa katika mchakato wa kuwania nafasi hiyo miaka mitatu ijayo.
Wengi wa wabunge wa chama hicho walioulizwa kutoa maoni yao kuhusu kauli hiyo ya Polepole waligoma kuzungumza wala kutajwa majina, huku wachache waliokubali kuzungumza wakiwa ‘makini na kauli zao’ jambo ambalo limetafsiriwa kuwa ni kutokana na hofu ya kuogopa kuonekana wasaliti.
Pengine kwa kutoamini msimamo huo wa Polepole, mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe aliuliza kupitia mtandao wake wa twitter, “hpolepole kaka hii ya Times FM kuwa 2020 mbunge lazima awe anaishi jimboni kwake ni kauli yako comrade”.
Ukiondoa swali hilo la Bashe, wabunge wengine hawakuwa tayari kuzungumzia lolote kuhusu msimamo huo wa Polepole kwa madai walikuwa hawajamsikia ‘mwenezi’ huyo wa CCM.
Mbunge wa Songwe, Phillip Mulugo alisema hataweza kuzungumzia suala hilo kwa sababu hakusikia lililozungumzwa. “Sikusikia ilipozungumzwa kwa hiyo sitaeleza chochote,”alisema.
Wakati wabunge wengine simu zao ziliita bila kupokelewa, mbunge wa Jimbo la Manonga, Seif Khamis Gulamali simu yake ilikatika kabla ya kutoa maoni na baadaye haikupatikana tena.
Baadhi ya wabunge wanaoishi katika majimbo yao, waliunga mkono kauli hiyo ya Polepole.
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alisema uamuzi huo ni sahihi kwa kuwa sababu kubwa ya rushwa kwenye chaguzi za CCM ni watu wasiojulikana kwa wananchi kujiuza kwa kutumia fedha.
Lusinde, ambaye ni miongoni mwa wabunge wanaoishi kwenye majimbo yao alisema wagombea ambao hurejea majimboni kutoka nje ya maeneo wanayoishi mara nyingi hutumia rushwa kuwahonga wananchi kama njia pekee ya kujitambulisha.
“Mtu kutoka Dar es Salaam asiyejua matatizo ya wananchi anawezaje kuwaongoza? Suala hili ni zuri kabisa na hakika litakomesha kabisa rushwa,” alisisitiza.
Mbunge huyo mwenye michango tata bungeni alisema wananchi wanahitaji viongozi wanaotoka miongoni mwao kwa kuwa wanafahamu changamoto na kero zinazowakabili hivyo akaunga mkono msimamo uliotolewa na Polepole.
Mmoja wa wagombea wa nafasi ya ubunge awamu zilizopita katika Jimbo la Iringa Mjini, Fadhil Ngajilo alisema japo anaunga mkono kauli hiyo, lakini chama hicho kinapaswa kufanya tathmini kwani zipo baadhi ya nafasi ambazo haziwalazimishi wagombea kuishi ndani au nje ya eneo husika ikiwamo ubunge.
Alisema kutoruhusu wakazi wanaoishi nje ya eneo husika kuwania nafasi ya uongozi kwenye eneo jingine ni sawa na kujifungia ndani ya boksi wakati utandawazi unamruhusu Mtanzania kuishi popote.
“Ni wazo zuri, lakini niwashauri viongozi wangu kwamba ziwepo nafasi zitakazoruhusu mtu kutembea kutokana na utandawazi. Mfano nafasi za ujumbe au hata ubunge. Lakini kwa wabunge wakishapata uongozi, basi kuwepo na sheria wawe wakazi wa eneo hilo,” alisema.
Ngajilo alisema hatari ya kutaka wakazi wa eneo husika ndio wawanie nafasi mbalimbali za uongozi kwenye maeneo yao kutasababisha kupatikana kwa wagombea wasio na ufahamu wa mambo mbalimbali (exposure) jambo ambalo ni hatari kulingana na hali halisi ya ushindani kwenye siasa.
Alieleza kuwa CCM inaweza kupata wagombea watakaoshindana na upinzani ikiwa watapewa wigo mpana badala ya kufungiwa.
Si wanasiasa tu walioguswa na kauli ya Polepole, hata wasomi na wadau walikuwa na maoni yao.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alisema uamuzi huo umechelewa kwa sababu ni ukweli usiopingika kwamba, wagombea wa nafasi za uwakilishi wa wananchi wanatakiwa kutoka miongoni mwao.
Profesa Bana alisema cheo chochote chenye dhana ya uwakilishi ni lazima wagombea wake watoke miongoni mwa wananchi.
“Mgombea akitoka mbali huyo lazima atumie rushwa na hatari yake ni kutofanya kazi ya uwakilishi aliyopewa kwa sababu akishashinda anaweza kutokomea. Si amenunua uongozi na tumeshuhudia baadhi ya watu huwa hawarudi, ukimtafuta,” alisema.
Alisema ni wakati muafaka kwa vyama vyote kuwa na kanuni itakayowalazimisha wagombea wake kutoka miongoni mwa wananchi wanaotaka kuwawakilisha.
Kama ilivyo kawaida kwa wasomi, Profesa Bana alipata mawazo kinzani kutoka kwa msomi mwingine.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Dk Jimson Sanga alisema wananchi wanapaswa kuachwa waamue mgombea wanayemtaka bila kujali sehemu anayotokea au anayoishi.
“Falsafa za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere zilishapiga vita ukabila, sasa kauli hii ya kutaka wagombea watokee kwenye eneo wanaloishi binafsi siungi mkono hata kidogo. Kama wao wamegundua mtu anayeishi Singida anaweza kugombea Njombe na anazijua shida zao kuwa ataweza kuzisema, aachwe agombee,”alisema.
Msimamo huo wa Polepole haukuishia katika maoni hayo ya wasomi na wanasiasa tu, ulikumbushia mchakato wa katiba mpya.
Mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano, uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema anaishangaa CCM kwa hatua yake ya kuchomoa kipengele kimoja baada ya kingine kutoka kwenye Rasimu ya Katiba ya Warioba wakati walishaikataa.
“Hilo la wabunge kutoka kwenye maeneo ya wananchi lipo kwenye rasimu ya Katiba ya Warioba. Tunamshangaa Polepole na CCM yake, nadhani kwanini wanataka kutumia vifungu vidogo vya rasimu? Watuletee rasimu nzima tuipitishe ili vyama vyote, tujue haya ndiyo maoni ya wananchi tuyafanyie kazi,” alisema Mrema.
Alisema badala ya kuendelea kunyofoa vifungu hivyo, ni vizuri waache mchakato wa kuipata Katiba mpya uendelee.
Naye Wakili wa kujitegemea, Harold Sungusia alisema kisheria vyama vya siasa vina taratibu zake za kupata wagombea wake.
Alieleza kuwa ukweli ni kwamba bado mfumo wa demokrasia ndani ya vyama vingi unatatizo katika kuwapata wagombea hao huku wanawake, wakiwa wahanga zaidi.
“Sheria inasema mgombea awe amedhaminiwa na chama cha siasa kwa hiyo, kila chama kina taratibu zake za kuwapata wagombea kwa hiyo mfumo uliopo ni wa ukiritimba,” alisema wakili hiyo.
Alieleza kuwa suluhisho la hayo yote ni sheria hiyo kuruhusu mgombea binafsi kwa sababu tayari Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu iliandika historia baada ya kutoa hukumu iliyohitimisha safari ndefu ya wananchi kutaka wagombea binafsi waruhusiwe katika chaguzi za serikali za mitaa, ubunge na urais.
Chanzo: Mwananchi