Ufaulu umepanda kwa zaidi ya asilimia mbili, mwaka 2015 ukiwa asilimia 67.84, mwaka 2016 (asilimia 70.36) na mwaka 2017 (asilimia 72.76).
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), wanafunzi 662,035 kati ya 909,950 waliofanya mtihani wa darasa la saba, wamefaulu.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana, katibu mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde alisema watahiniwa waliofaulu wamepata alama 100 au zaidi kati ya alama 250 wanazopaswa kupata.
Msonde alisema idadi hiyo ya waliofaulu ni sawa na asilimia 72.76. Alisema kati yao wasichana ni 341,020 ambao ni sawa na asilimia 70.93 na wavulana ni 321,015 (asilimia 74.80).
Dk Msonde alisema mwaka 2016 waliofaulu walikuwa asilimia 70.36, hivyo kuna ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.40.
Akizungumzia takwimu za matokeo, Dk Msonde alisema ufaulu katika masomo ya Kiswahili, Kiingereza na Hisabati umepanda kwa asilimia kati ya 4.25 na asilimia 10.05 ikilinganishwa na mwaka 2016.
“Kwa masomo ya Sayansi na Maarifa ya Jamii, ufaulu umeshuka kwa asilimia kati ya 3.56 na asilimia 13.97 ikilinganishwa na mwaka 2016,” alisema.
Dk Msonde alisema watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili, ambalo kiwango cha ufaulu ni asilimia 86.86, lakini kiwango cha Kiingereza ni asilimia 40.30.
Katika matokeo hayo, Msonde alizitaja shule 10 bora kitaifa kuwa ni St Peter, St Severine, Mwanga na Rweikiza zote za Mkoa wa Kagera, Alliance (Mwanza), Sir John (Tanga), Palikas (Shinyanga), Hazina na St Anne Marie (Dar es Salaam) na Martin Luther (Dodoma).
Dk Msonde alizitaja shule 10 ambazo hazikufanya vizuri kuwa ni Nyahaa, Mntamba na Ikolo zilizopo mkoani Singida, Bosha, Kishangazi na Mkulumuzi (Tanga), Ntalasha (Tabora), Kamwala (Songwe), Kibutuka (Lindi) na Kitwai A (Manyara).
Aliitaja mikoa 10 iliyoongoza kitaifa kuwa ni Dar es Salaam, Geita, Kagera, Iringa, Kilimanjaro, Njombe, Arusha, Mwanza, Katavi na Tabora.
Dk Msonde aliwataja watahiniwa 10 bora kuwa ni Hadija Azizi Ally, Naseem Kareem Said na Insiyah Kalimuddin wote kutoka shule ya Sir John.
Wengine ni Ibrahim Shaban kutoka shule ya Tusiime, Kadidi Mkama Kadidi (Paradise), Mahir Ally Mohamedy na Mbarak Faraj (Feza), Colletha Masungwa na Philimon Damas (St Achileus) na Acius Job Missingo (St Peter Claver).
Aliwataja wasichana 10 bora kitaifa kuwa ni Hadija Azizi Ally, Naseem Kareem Said, Insiyah Kalimuddin, Linah John Lameck, Saada Ahemd Omary na Khadija Salim Omary wote kutoka shule ya Sir John; Colletha Masungwa (St Achileus), Hannat Ramadhani (Dar-Ul-Muslimeen), Efrosina Geofrid (Omukaliro) na Nancy Elirehema Mejooli (Tusiime).
Wavulana 10 bora kitaifa ni Ibrahim Shaban wa Tusiime, Kadidi Mkama Kadidi (Paradise), Acius Job Missingo (St Peter Claver), Mahir Ally Mohamedy (Feza), Mbarak Faraj (Feza), Philimon Damas (St Achileus), Huruma Godfrey (Mwanga), Hamza Azael Almas (Hazina), Gobbons Roy (Fountain of Joy) na Erastus Joseph (St Peter Claver).
Dk Msonde alizitaja halmashauri 10 zilizoongoza kitaifa kuwa ni Kinondoni, Moshi, Arusha, Ilala, Mafinga Mji, Mlele, Kigamboni, Nzega Mji, Mpanda na Chato.
Katika hatua nyingine, Necta imezuia matokeo ya watahiniwa 65 waliougua au kupata matatizo na kushindwa kufanya mitihani yao yote au baadhi ya mitihani.
Wanafunzi hao wamepewa fursa ya kufanya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi mwakani.
Necta pia imefuta matokeo yote ya watahiniwa 10 waliofanya udanganyifu.