Klabu ya soka ya Ndanda FC imesema haitambui mikataba iliyosainiwa na Kamati iliyokuwa ikiendesha timu kabla ya kuirejesha kwenye bodi takribani miezi miwili iliyopita.
Msemaji wa Ndanda FC Idris Bandali amesema kuwa tangu kamati hiyo irudishe timu haijawasilisha mikataba waliyoingia na makampuni mbalimbali ikiwemo Maxcom Limited na Kiboko.
“Klabu ya Ndanda haina nia mbaya na wadhamini lakini tunachotaka sisi wale watu walioingia nao makubaliano watuletee hizo taarifa walete mikataba”, amesema Bandali.
Aidha Bandali ameongeza kuwa taarifa ya Mhasibu wa Ndanda imesema akaunti ya timu haina pesa yoyote iliyoingia kutoka kwa hao wadhamini hivyo hawawezi kuendelea kukaa na mabango ya makampuni hayo uwanjani hivyo lazima wayatoe ili yasije kuleta utata baadae.
Kamati hiyo pia imedaiwa kusajili wachezaji na kuwapeleka Ndanda bila kuwasilisha mikataba yao kwa timu na shirikisho kitu ambacho ni kinyume na sheria za soka. Kwa mujibu wa Bandali kamati hiyo imeitwa mara nyingi na kuombwa kuwasilisha mikataba lakini imekuwa haitaki kuitikia.