Kujiuzulu kwa Kocha Mayanja Kwawavuruga Simba

Kujiuzulu kwa Kocha Mayanja Kwawavuruga Simba
Sakata la kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja kutangaza kubwaga manyanga limeibua mshangao huku kaimu rais wa Simba, Salum Abdallah ‘Try again’ akizungumza chemba na kocha huyo Mganda jana mchana bila kuwa na taarifa.

Habari za kocha huyo msaidizi wa Simba kujiuzulu zilianza kusambaa jana asubuhi kwenye mitandao ya kijamii, huku mabosi wa Simba wakiwa hawafahamu chochote.

Gazeti hili lilimtafuta kaimu rais wa Simba, Salim Abdallah kama wamepewa taarifa rasmi na kocha huyo lakini, alionyesha sintofahamu juu ya taarifa hiyo.

Wakati akionyesha kutofahamu, Abdallah alikuwa na Mayanja wakati huo wakizungumza bila kujua kuwa anayezungumza naye ana mpango wa kuachia ngazi.

“Mayanja kujiuzulu? Mbona niko naye hapa, unataka nikupe umsalimie?,” Aliuliza bosi huyo wa Simba na mwandishi alikubali na kaimu rais huyo alimpa Mayanja simu.
Mayanja, licha ya kuwa hadi wakati huo hakuwa amemwambia bosi huyo uamuzi wake, alikiri mbele yake kuwa anadhamiria kubwaga manyanga, jambo lililomshitua Abdallah, ambaye ana kaimu nafasi ya Evans Aveva.

Licha ya kwamba inaelezwa Mayanja ametangaza kujiuzulu kutokana na maneno kuzidi kwenye timu yao, mwenyewe hakuwa tayari kuzungumzia chanzo cha kuachana na timu hiyo.

“Ni kweli kinachozungumza ndicho kipo, lakini siwezi kulisemea hilo mimi, uongozi utatoa tamko,” alisema Mayanja kupitia simu ya rais wa Simba, ambaye naye alisisitiza suala hilo litatolewa ufafanuzi na msemaji wao Haji Manara.

“Sikuwa najua chochote hadi wakati huu licha ya kuwa na Mayanja hapa, lakini ngoja nimsikilize kisha ufafanuzi wote utatolewa na ofisa wetu wa habari, Manara,” alisema Abdallah.

Alipotafutwa Manara baadaye kwa ajili ya kufafanua hilo, alisema taarifa aliyoitoa Mayanja katika ukurasa wake wa Instagram ilijitosheleza na wao kama uongozi utakaa kabla ya kutoa ufafanuzi.

Kama ulivyoona alichoandika katika Instagram, amefikia uamuzi huo yeye, nasi hatuna cha kuongeza hapo kwa sasa ila tutatoa taarifa yetu,” alisema Manara bila kusema siku atakayotoa taarifa hiyo Katika ukurasa huo wa Mayanja, kocha huyo raia wa Uganda aliandika kwa kifupi juu ya kuachia ngazi akitaja sababu binafsi ndizo chanzo cha kuchukua uamuzi huo.

Makocha washangazwa

“Hii kama hadithi, Mayanja kaondoka Simba! daaah! Lakini ndiyo mpira wa kibongo ulivyo,” alisema kocha wa Stand United, Athuman Bilal ‘Bilo’.
Kocha wa Njombe Mji, Mrage Kabange alisema anashangazwa na uamuzi huo kwani Simba haipo katika nafasi mbaya kwenye msimamo kiasi cha kufanya uamuzi mgumu.

“Unajua kama ingekuwa ya mwisho au inaning’inia kwenye msimamo sawa, lakini mmmh! Tuwaachie wenyewe,” alisema Kabange kwa kifupi.
Wakati kocha wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila akisema timu hiyo iachwe kama ilivyo kwani Simba na Yanga katika soka hazitabiriki.

Jackson Mayanja alizaliwa Julai 27, 1969 nchini Uganda, ni fulubeki wa kulia kuwahi kushuhudiwa nchini humo kwa wakati wake.

Mayanja ni maarufu kwa jina la Mia Mia (100%) nchini kwao, ambalo alipewa wakati anacheza El Masri ya Misri 1992.

Jina hili lilitokana na kila alichokuwa akifanya uwanjani alikuwa hakosei, alikuwa na pasi sahihi fupi na ndefu na kuwashawishi Waarabu kumpa jina hilo kama mtu sahihi kwa kila afanyacho uwanjani kinafanikiwa kwa asilimia 100.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad