KOCHA Mkuu wa Yanga, Mzambia, George Lwandamina, amefungukia pengo la straika wake, Amissi Tambwe, raia wa Burundi. Tambwe ambaye msimu uliopita alifunga mabao 12 katika Ligi Kuu Bara, msimu huu kwake umeanza vibaya baada ya kushindwa kucheza hata mechi moja kati ya tano za ligi walizocheza wenzake.
Kukosekana kwa Tambwe ambaye alikuwa akiuguza majeraha ya goti, inaonyesha kwamba inachangia uhaba wa mabao ndani ya kikosi hicho kwani katika mechi hizo tano, Yanga imefunga mabao manne pekee tofauti na msimu uliopita ambapo katika mechi kama hizo, timu hiyo ilikuwa imefunga mabao nane huku Tambwe akifunga matatu.
“Ni kweli Tambwe tumemkosa katika mechi hizi za mwanzo, lakini kukosekana kwake haiwezi kuwa tatizo kwa sababu kuna wengine wanacheza nafasi yake kama Obrey Chirwa.
“Anapokosekana mchezaji mmoja kikosini huwa hakuna pengo kutokana na kwamba hapa wote wanaelewana vizuri na kila mmoja anajua majukumu yaike, hivyo akipewa nafasi anafanya vizuri,” alisema Lwandamina.
Daktari wa Yanga, Edward Bavu, alisema leo Jumatatu Tambwe anaanza mazoezi ya nguvu na atakuwa fiti kucheza mchezo ujao dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa Oktoba 13 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Stori: Omary Mdose