Kocha mkuu wa klabu ya Yanga, George Lwandamina amethibitisha kuwa kikosi chake kipo tayari kuivaa Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara VPL leo jioni kwenye uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Akizungumza katika mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo, Lwandamina amesema wachezaji wake wote wapo vizuri kuivaa Kagera ambayo itakuwa nyumbani.
Pamoja na kuwakosa wachezaji wake watatu, kiungo Thabani Kamusoko, mshambuliaji Donald Ngoma na mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe lakini bado Lwandamina ana imani na wachezaji wengine waliopo kwenye kikosi chake.
“Timu yetu inawakosa Tambwe, Ngoma na Kamusoko, lakini bado timu yetu ina kikosi cha kutosha na nina imani na wachezaji wote wanaweza kufanya vizuri,”amesema Lwandamina.
Ukiacha mchezo wa Yanga, Ligi Kuu itaendelea leo kwa mechi zingine nne ambapo Mwadui FC wataikaribisha Azam FC Uwanja wa Mwadui Complex, Ndanda watawakaribisha Maji Maji ya Songea, wakati Singida United itacheza na wenyeji Ruvu Shooting ya Pwani. Njombe Mji na Lipuli ya Iringa watacheza kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.