Mahakama ya Wilaya ya Ilala imemkuta na kesi ya kujibu mshtakiwa Salum Njwete maarufu kama Scorpion anaekabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kujeruhi ambae aliingia kwenye vichwa vya habari baada ya kumtoboa mtu macho.
Hatua hiyo inatokana na Hakimu Mkazi Flora Haule kusema kuwa amepitia ushahidi wa upande wa mashtaka na kujiridhisha na kuona mshtakiwa Njwete ana kesi ya kujibu.
Hakimu Haule amesema kwa sababu hizo, Mshtakiwa anapaswa kutoa utetezi kwa njia atakazopenda kama kwa kiapo ama bila kiapo ambapo baada ya kueleza hayo, Mshtakiwa Njwete alisema kuwa atajitetea mwenyewe kwa njia ya kiapo lakini pia atakuwa na mashahidi wawili ambao walitumiwa kama Mashahidi wa upande wa mashtaka jambo ambalo Hakimu Haule amelikataa na kusema atafute mashahidi wengine au ajitetee mwenyewe.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Njwete anaetetewa na wakili Juma Nassoro anaidaiwa Septemba 6, 2016 saa 4 usiku maeneo ya Buguruni Ilala Dar es Salaam, aliiba cheni ya Silva yenye uzito wa gramu 34 ikiwa na thamani ya Sh 60,000 na simu ya mkononi pamoja na fedha taslimu Sh 330,000 vyote vikiwa na thamani ya Sh 474,000 mali ya Said Mrisho Said.
Pia anadaiwa kabla na baada ya kutekeleza tukio hilo, Mtuhumiwa huyo alimchoma Mrisho sehemu mbalimbali za mwili wake ikiwemo machoni, tumboni na mabegani ili kurahisisha kupata mali hizo.
Hakimu Haule ameahirisha kesi hiyo hadi November 14, 2017 kwa ajili ya Njwete kuanza kujitetea.
Mahakama Yamkuta na Kesi ya Kujibu 'Scopion' Atakiwa Kujitetea Novemba 14
0
October 31, 2017
Tags