Makamu wa Rais Awaonya Trafiki Wanaogeuza Touch za Barabarani Kuwa Mtaji
0
October 17, 2017
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaonya Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani kuacha kugeuza vifaa vya kupimia mwendo wa magari maarufu kama tochi, kuwa chanzo cha wao kujipatia rushwa.
Mama Samia Suluhu ameyaeleza hayo leo wakati akifungua maadhimisho ya wiki ya nenda kwa usalama ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Kilimanjaro.
Makamu wa Rais amewataka trafiki kujiepusha na vitendo vya rushwa na badala yake watilie mkazo katika ulinzi wa usalama na usimamizi wa sheria za barabarani.
Pia, amewataka kutowanyanyasa madereva ambao wanazingatia sheria za usalama barabarani.
Samia alieleza kuwa 76% ya ajali za barabarani huchangiwa na makosa ya kibinadamu ikiwamo madereva kuendesha magari huku wakitumia simu zao, uchovu unaosababisha madereva kusinzia, pamoja na kuendesha wakiwa walevi.
Aliendelea kwa kusema ubovu wa miundombinu ya barabara pamoja na ubovu wa magari nayo imechangia kutokea kwa ajali za barabarani kwa asilimia 16.
Vile vile alieleza kuwa kukosekana kwa umakini na uzembe wa madereva wa bodaboda kumepelekea kuongezeka kwa idadi ya ajali za barabarani ambako kungeweza kuepukika.
Samia amesema Taifa limeendelea kupoteza nguvu kazi, watu kupata ulemavu wa maisha na wengine kubaki wajane.
“Mwaka huu kuanzia Januari hadi Septemba kumekuwa na ajali za pikipiki 42,721 zilizoua watu 1,613 na kusababisha majeruhi 1,597,” amesema.
Amesema Mkoa wa Kilimanjaro umeripotiwa kuwa na ajali 84 za bodaboda zilizosababisha vifo 61 na majeruhi 21.
Samia ameeleza kusikitishwa kwa Tanzania kutajwa katika ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa ni nchi inayoongoza kwa ajali ikiwa na asilimia 33.
Ameliagiza Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani na wadau kuzingatia na kuelekeza nguvu kwenye kudhibiti makosa makubwa matano hatarishi.
Makosa yaliyotajwa ni pamoja na mwendo kasi, ulevi, kutovaa kofia ngumu, kutovaa mikanda ya usalama katika gari na ukosefu wa vifaa vya usalama kuwalinda watoto wadogo wakiwa ndani ya gari.
Tags