WATU watatu kati ya sita waliokuwa wakisafiri na malori yanayomilikiwa na kiwanda cha saruji cha Dangote mkoani Mtwara, wamekufa papo hapo na wengine kulazwa Hospitali ya Sokoine ya mkoa wa Lindi, baada ya magari hayo kugongana uso kwa uso.
Waliofariki ni Issa Rashidi Mbweso (28) ambaye ni dereva wa lori namba T 481 DJZ na mkazi wa mjini Mtwara, Haruni Nazir Mbonde (48) ambaye pia ni dereva wa lori la kiwanda hicho pamoja na utingo wake aliyefahamika kwa jina moja la Rajabu.
Majeruhi ni Ramadhani Nasoro (30) utingo na mkazi wa mjini Mtwara, Sophia Isumaili (35) na dada yake, Mawazo Omari (40) wakazi wa Kata ya Mandawa wilaya ya Kilwa.
Wakizungumza na Nipashe katika hospitali hiyo Lindi, majeruhi hao akiwamo utingo wa lori hilo namba T 481 DJZ lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Mtwara, walisema ajali hiyo ilitokea eneo la kitongoji cha Mihambwe, kwenye barabara kuu ya Kibiti-Lindi juzi mchana.
Sophia Isumaili na dada yake Mawazo Omari waliokuwa wameomba lifti kutoka Mandawa kwenda Newala mkoani Mtwara, walisema walipofika kitongojini hapo na kukuta barabara imezibwa na wingu la moshi mzito, alimuomba dereva Issa ambaye ni marehemu asimamishe gari wasubiri kupungua kwa moshi huo, lakini alikaidi na kujitosa.
“Tulipofika eneo lile na kukuta moshi mwingi nilimshauri dereva wetu tusimame ili kupisha moshi, lakini hakuwa tayari na kujibu atapita tu bila shida,” alisema Sophia.
Utingo Ramadhani Omari alisema kutokana na dereva kukaidi ushauri huo, walijikuta wakigongana uso kwa uso na lori lingine lililokuwa limebeba saruji likiwa limesimama kando ya barabara kupisha kupungua kwa moshi huo.
Alisema baada ya malori hayo kugongana, kulijitokeza cheche za moto na kuteketea kwa magari yote hayo wakiwamo madereva na utingo, kabla ya gari la Zimamoto kutoka Manispaa ya Lindi kwenda eneo la tukio Mihambwe kuuzima moto.
Mganga wa zamu katika Hospitali ya Sokoine, Dk. Edgal Mlawa, alithibitisha kupokea miili na majeruhi watatu, lakini hakuwa tayari kutoa maelezo zaidi akisema hadi mkuu wake wa kazi atakapofika.
“Licha ya kuwa nipo zamu muda huu, lakini siwezi kuelezea zaidi kwani mwenye mamlaka ya kuzungumza na vyombo vya habari ni mkuu wangu wa kazi,” alisema Dk. Mlawa.
Kamanda wa Polisi mkoani Lindi, Renatha Mzinga, alipoulizwa kupitia simu yake ya mkononi, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza taarifa kamili ataitoa baada ya kupelekewa na vijana wake waliokuwapo eneo la tukio.