Mambo 6 ya Msingi ya Kufahamu Kabla ya Kupekuliwa na Polisi
0
October 11, 2017
NA BASHIR YAKUB –
Unapopekuliwa yapo mambo ambayo usipoyazingatia wewe unayepekuliwa basi yatakuingiza matatani mbeleni au hata kama umebambikiziwa kosa itaonekana ni kweli na waweza kwenda jela bila kuwa umetenda kosa lolote.
Kawaida wanaopekua ni askari. Usitarajie huyu anayekuja kukupekua awe ndiye wa kukwambia haki zako . Badala yake wewe unayepekuliwa ndiye uwe wa kumwambia askari kuwa hiki ndicho hiki hapana. Askari anapokuja kukupekua tayari wewe unashukiwa na hivyo ni rahisi kwake kuacha kufuata au kuongeza jambo lisilokubalika ilimradi atimize lengo lililomleta. Wewe ndiye wa kusema hili ndio na hili hapana.
Hivyo basi ni muhimu sana kwako kujua kuhusu kupekua na mambo gani ya msingi ufanyiwe au usifanyiwe ili kuepuka uwezekano wa kwenda jela bila kosa.
Usiseme mimi sina haja ya kujua kuhusu kupekua kwasababu ni mwema sana na hivyo si rahisi kutakiwa kupekuliwa. Laa hasha, kupekuliwa na kukamatwa na polisi humkumba yeyote awe mwema ama vinginevyo. Kujua ni silaha na hivyo ni muhimu kukaa na silaha hii.
Makala yatapitia sura ya 20, vifungu vya 38 hadi 45 vya Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai .
ANARUHUSIWA KUKUPEKUA.
Askari ndiye anayeruhusiwa kukupekua. Hata raia wanaweza kumzuia raia mwenzao wakampekua ikiwa wana taarifa kuhusu kuficha au kumiliki kitu ambacho ni kosa kwa mujibu wa sheria. Isipokuwa ni haramu kabisa kwa raia kumpekua raia mwenzake bila kuwa na kibali maalum.
VITU GANI VINAWEZA KUPEKULIWA.
Mtu kama mtu anaweza kupekuliwa, kwa maana nguoni mwake kama mifukoni nk. Pia vifaa kama gari, ,meli, nk navyo vyaweza kupekuliwa. Halikadhalika nyumba kama nyumba nayo yaweza kupekuliwa pamoja navyo vifaa vingine.
JE WAWEZA KUPEKULIWA MDA WOWOTE.
Hapana, si kweli kuwa waweza kupekuliwa mda wowote anaotaka askari. Sheria niliyotaja hapo juu inasema mda wa kupekua ni kuanzia jua linapochomoza na mwisho ni linapozama. Yametumika maneno jua kuchomoza na kuzama badala ya kutaja mda labda saa 11 za asubuhi mpaka saa 12 za jioni kwasababu ya utofauti wa jiografia ya sehemu na sehemu.
Muonekano wa saa 12 za jioni wa kanda ya ziwa ni tofauti na ule wa pwani nk. Kwahiyo kutaja saa kwa lengo la kumaanisha usiku unapoingia na unapotoka ingekuwa kama inapotosha.
Hata hivyo inawezekana tu kupekuliwa nje ya muda huo kwa kibali maalum cha mahakama.
MPEKUAJI KUAMBATANA NA SHAHIDI MWENYEJI.
Askari anayepekua aje na shahidi mwenyeji. Mjumbe au kiongozi kutoka serikali za mitaa ni mtu muhimu kuwa mwenyeji. Jirani pia anaweza kuwapo. Hii ni kuhakikisha wanakuwa mashahidi kuwa hakuna kilichoingizwa ndani wakati kuingia kupekua na pia kushuhudia vinavyochukuliwa.
ORODHA YA VITU VINAVYOCHUKULIWA.
Ni lazima kila kinachochukuliwa kuandikwa kwenye orodha maalum . Orodha hiyo utaisaini wewe uliyepekuliwa, askari aliyekupekua, pamoja na mashahidi ambao ni mjumbe au serikali za mitaa au jirani mwema.
Hii huepusha badae kuambiwa kuwa hata kitu fulani ambacho kinajenga kosa kuwa kilikutwa kwako. Lakini pia ni muhimu kwa ajili ya kurejesha mali zako baadae zikiwa zimetimia.
KIBALI CHA KUPEKUA.
Askari mwenye cheo chini ya Sub Inspector haruhusiwi kupekua nyumba au eneo la mtu bila kibali maalum aidha kutoka mahakamani au kutoka kwa mkubwa wake mwenye cheo cha Sub Inspector kwenda juu. Hii ni kwa kesi ya kupekua nyumba.
Kwa kesi ya kupekua mtu binafsi pale anaposimamishwa au upekuzi wa gari na vifaa vingine askari yeyote anaweza kupekua bila kibali.
Tags