Mambo Usiyopaswa Kufanya Kwenye Kundu la Whats App


Katika nyakati tunazoishi sasa mawasiliano yamekuwa jambo jepesi na rahisi kuliko hapo awali. Tofauti na wakati wa kutumiana barua kupitia posta ambapo barua ilikuwa inaweza kuchukua mpaka mwezi mzima pasipo kumfikia muhusika.

Matumizi ya simu na tarakilishi (computer) pamoja na mtandao (internet) kumeyafanya mawasiliano kuwa rahisi sana. Hii imepelekea wataalamu kuunda programu mbalimbali za kurahisisha mawasiliano baina ya watu wawili au zaidi wanaotumia simujanja (smartphone) au tarakilishi (computer).

Programu hizo ni kama vile WhatssApp, Telegram, Twitter, instagram, facebook na nyingine nyingi.

Imefikia hatua mpaka programu hizo zinawawezesha watumiaji wake kuunda makundi ya majadiliano na mazungumzo.

Katika kundi kunakuwa na watu wengi na wenye imani, malezi, uwezo, elimu na tabia tofauti tofauti.

Ili kuepuka kuonekana kikwazo au kero katika makundi ya majadiliano ya mitandaoni kama ‘whatApp groups’ inabidi uyazingatie yafuatayo;

Usitumie majina ya kejeli

Tumia majina ya utani na ya kusisimua lakini angalia kwa pande zote, isije ikawa jina unalolitumia linawakwaza wengine. Kumbuka ni kundi la ‘kuchati’ na hauko peke yako.

Usitume jumbe zenye maneno mengi

Ukweli ni kwamba jumbe zenye maneno mengi huwa hazisomwi na huwakera watu wengi. Hivyo ili kuepuka kuwakera wengine na kuonekana msumbufu basi tumia maneno machache kueleza ujumbe wako. Vile vile kama ujumbe unaoutuma una jambo la muhimu unalotaka watu wengine walifahamu, kuna uwezekano mkubwa wasilifahamu kama una maneno mengi. Jitahidi kufupisha. @swahilitimes.com

Usijiondoe (left) kwenye kundi pasipo taarifa

Kabla ya kujiondoa katika kundi hakikisha kuwa unatoa taarifa kwa wanakikundi na ikiwezekana uwaambie sababu ya kujiondoa ili watambue kuwa hautokuwepo nao tena. Siyo vizuri ‘kuleft’ pasipo taarifa.

‘Usi-screenshot’ chochote pasipo kuomba ruhusa

Watu wengi wamekuwa na tabia ya ‘ku-screenshot’ jumbe ama picha za wengine pasipo kuomba ruhusa kwa wahusika pasipo kujua kwamba ni kosa na ni kuhatarisha usalama wa wengine katika kundi. Acha tabia hiyo mara moja.

Usitume jumbe nyakati za usiku sana

Kuna watu wengi wamekuwa wakikesha ndani ya makundi ya whatsApp na kutumiana jumbe moaka saa 9 usiku. Unashangaa unaamka saa 12 asubuhi unakuta jumbe 1765 ambazo hukuziacha wakati ulipoenda kulala. Kwa wote wenye tabia ya ‘kuchat’ usiku wa manane wanapaswa kuiacha tabia hii kwani wengine nao wanahitaji muda mzuri wa kupumzika na kulala usingizi mwororo.

Usiwe mtazamaji

Kwenye makundi ya whatsApp kuna baadhi ya watu huwa ni watazamaji tu (observers). Watu wa aina hii huwa hawachangii chochote zaidi ya kuwa wanasoma jumbe za wengine na kucheka kimoyomoyo. Usiwe na tabia hii, hakikisha na wewe unashiriki mijadala mbali mbali inayoanzishwa na wengine katika kundi.

Usiligeuze kundi kuwa sehemu yako ya kupeleka malalamiko au ya kujisifia

Wako watu wanaoyageuza makundi ya whatsApp kama ‘therapy session’ ambapo wanaenda kujieleza mambo yote yanayowasumbua, namna maisha yanavyowaendea na magumu yote wanayoyapitia. Wengine hutumia makundi hayo kama sehemu ya kujisifia kuhusu wanalivyofanikiwa kimaisha, wanawake warembo waliokuwa nao, vyakula wanavyokula, maeneo ya starehe waliyohudhuria  na vingine vya kufanan na hivi. Kumbuka siyo kila mmoja anataka kusikia hayo malalamiko au sifa zako.

Usiiweke kazi yako hatarini kisa jumbe za makundi ya whatsApp

Utakuwa ni mtu wa ajabu sana kama utaamua kuendekeza na kuzipa kipaumbele ‘whatsApp charts’ kuliko kazi yako. Hakikisha kuwa ‘una-mute notifications’ za makundi yote pale unapokuwa na kazi muhimu za kufanya. Ukiendekeza sana whatsApp unajua kitakachokukumba pale utakapokamatwa na mkuu wako wa kazi. Utakapofukuzwa kazi, hakuna hata mmoja ndani ya kikundi atakayekuajiri. Fikiri kwa kina.

Usiwe mtoa taarifa kila mara

Baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya ‘ku-share’ jumbe, taarifa, sauti na video kila wanapoipata kutoka kundi lingine. Wengine wamekuwa na tabia ya kusema kila wanachokiona katika televisheni. Mfano watu wanaangalia mpira, mara goli linafungwa.. wewe haraka unakimbilia kwenye kundi kutoa taarifa. Usione watu wamekukalia kimya ukadhani wanafurahishwa. Pengine wanadharau unachokifanya na kukuona usiye na akili. Jaribu kutokuonekana kero kwa wengine.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad