HIVI karibuni ulisambazwa waraka mzito na wa kushtua kwenye mitandao ya kijamii uliosemekana umeandikwa na mwanamuziki wa dansi mkongwe nchini, Nguza Viking almaarufu kama Babu Seya anayekitumikia kifungo cha maisha gerezani.
Kufuatia kusambaa kwa waraka huo, Gazeti la Uwazi mwishoni mwa wiki iliyopita liliingia katika Gereza la Ukonga jijini Dar anapokitumikia kifungo chake mwanamuziki huyo na kuzungumza naye ambapo alianika mambo mapya mbali na waraka huo.
WARAKA ULIOSAMBAA
Waraka huo wenye ujumbe mzito uliodaiwa uliandikwa ili umfikie Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ ulisomeka hivi:
“MFUNGWA WA MAISHA
Na Babu Seya akiwa gerezani
…NAWAOMBA Mwambieni Rais Magufuli juhudi zake nazisikia.
“Mungu azidi kumpa maarifa zaidi kuliongoza vyema jahazi la Watanzania.
“Rais huyu nimependa hekima zake.. Mimi namfananisha na mwandishi wa makala za kitabu cha methali na Mhubiri Nabii Suleiman.
“Mwambieni rais nimeiweka akiba yangu ya tumaini la mwisho kwake, kwani MUNGU NDIYE MFALME WA KWANZA AWEZAE KUMALIZA MSIBA WANGU HUU WA KUISHI KWENYE KUTA ZA GEREZA.
Wa pili ni yeye RAIS JOHN JOSEPH awezae kunitenganisha mimi na maisha ya gereza.
“Sipendi ndoto yangu ya kuja kufia gerezani…naichukia kama tawala za Herode pale Galilaya. Naumwa huku hakuna makaburi mazuri ya kuzikia wafu wetu.
“ Mwambieni anisaidie japo nije kufia kwenye mikono ya mama yangu tu aliyeteseka leba kwa kumwaga damu yake nyingi wakati wa kunizaa…
“Kama ikishindikana siyo mbaya… U can see my dead body through my window coffin.
“Mtaweza kushuhudia maiti yangu yenye pamba masikioni na puani ikiwa ndani ya jeneza langu kupitia upenyo finyu wa dirisha la jeneza hilo…
“Nimekinai na hukumu na nimeshajifunza mengi. Siku nitakayotoka ndiyo siku nitakayolivaa joho la uchungaji na kupita mitaani nikihubiri neno la Mungu mpaka jasho langu ligeuke damu!
“Natumaini katika mkono wa bwana na natumaini katika mkono wa John Joseph. Halelujah, tutaonana madhabahuni…” ni sehemu ya waraka huo unaodaiwa kuwa ni wa Babu Seya.
UWAZI LATINGA GEREZA LA KEKO
Baada ya kuuona waraka huo Gazeti la Uwazi lilifunga safari hadi Gereza Kuu la Ukonga ililopo Wilaya ya Ilala jijini hapa, ambapo lilikutana na ulinzi mkali na sheria kali za gereza hilo.
Hata hivyo, lilifanikiwa kuonana na Mkuu wa Gereza, ACP Stephen Mwaisabila ambaye alisema:
“Waraka huo haujaandikwa na Babu Seya kwa sababu kuna utaratibu maalumu wa wafungwa kuandika barua kwenda kwa viongozi au sehemu yoyote wanayotaka waraka wao ufike.
“Inashangaza kuona kuna watu wanafanya kitu kama wafungwa, kwa kuandika uzushi mbalimbali kuhusu Babu Seya, kwani kuna wakati walivumisha kuwa Babu Seya kaachiwa, wengine walimuona hospitalini akipita wakavumisha kuwa yuko hoi.”
UTARATIBU WA KUANDIKA BARUA KWA WAFUNGWA
“Mfungwa yeyote ana haki ya msingi ya kuandika barua kwenda anapotaka lakini ni lazima barua yake ipitie kwa Mkuu wa Gereza, Mkuu wa Magereza wa Mkoa (RPO), Kamishna Jenerali wa Magereza (CGP), kisha inaenda kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, ndipo hupelekwa kwa kiongozi anayemtaka kama ni waziri mkuu au rais.”
Mkuu huyo wa gereza aliwaonya wanaondika uzushi huo kuwa, ni kosa kisheria kuandika mambo ya serikali wakati kuna watu walioaminiwa kwa ajili ya mambo hayo.
UWAZI ANA KWA ANA NA BABU SEYA
Uwazi lilimuona Babu Seya akiwasimamia kama kocha wafungwa wenzake ambao walikuwa wakicheza mpira wa miguu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 18 ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mwandishi wetu aliomba kumsalimia Babu Seya, aliruhusiwa akaambiwa hairuhusiwi kumpiga picha.
BABU SEYA AFUNGUKA
“Nikushukuru kwa kuja kunisalimia, ujumbe ambao unasema umeenea kwenye mitandao ya kijamii, sijauandika ila nafarijika kuona kuna watu wananipigania.
“Ombi langu ukitoka nje kupitia gazeti lako mwambie Mheshimiwa Rais Dk. John Pombe Magufuli namuomba alipitie upya faili letu.
“Ni kweli mahakama ilitukuta na hatia, hatuna uwezo wa kupinga hukumu iliyotolewa na mahakama lakini ombi langu kwa Rais Magufuli ninamuomba apitie upya faili letu, nasema kwa dhati, mimi sina hatia,”alisema Babu Seya.
Hii ni mara ya pili kwa gazeti hili kuzungumza na Babu Seya akiwa gerezani tangu ahukumiwe kifungo cha maisha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu zaidi ya miaka 10 iliyopita.