Kuelekea mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga, Jumamosi hii, wachezaji waliowahi kuzichezea klabu hizo, wameelezea namna ambavyo mashabiki wanaweza kuumizwa na matokeo yatakayokinzana na matarajio yao.
Hiyo ni kutokana na timu hizo kushinda kwa idadi sawa ya mabao kabla ya mchezo huo, Simba iliibuka na ushindi mnono dhidi ya Njombe Mji kwa mabao 4-0,huku Yanga wakishinda ugenini dhidi ya Stand United kwa mabao 4-0.
Sekilojo Chambua ni staa wa zamani wa Yanga, alielezea kuwa ; "Hii kila timu kushinda mabao sawa haina maana inaweza kubadili chochote kwenye matokeo zaidi ya kuleta hamasa na mchezo kuwa na presha kubwa, ila ninaloliona ni huku kwa mashabiki ambao wanatambiana kuona kila mtu anaweza kuibuka mshindi, wajiandae kisaikolojia."
Kwa upande wa Bitta John, nyota wa zamani wa Simba, alisema; "Labda kwa Yanga mchezaji tishio naona atakuwa Chirwa, lakini kikubwa makocha wanatakiwa kufanya kazi kubwa ya kuwajenga wachezaji wao kuwa makini wasije wakaingia kwa kuvimba kiasi kwamba wakasahau kazi yao mwisho wa siku wakavuruga mchezo."