Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi amesema haridhishwi na hali ya usafi wa mazingira wilayani humo, hivyo amewataka viongozi kuwajibika ipasavyo.
Amewataka watendaji wa kata kuongeza jitihada za kusimamia usafi ili kuepusha hatari ya kuibuka maradhi ya mlipuko kikiwemo kipindupindu.
Hapi akizungumza leo Jumanne wakati wa mkutano na viongozi, wakiwemo maofisa afya, watendaji kata na wenyeviti wa mitaa amesema baadhi ya maeneo yamekithiri kwa uchafu ukiwemo utiririshaji maji taka, huku baadhi ya mitaro ikiwa michafu kwa muda mrefu.
"Kila baada ya msimu wa mvua kinachofuata ni kipindupindu. Ni aibu kuwa na kipindupindu Kinondoni," amesema.
Amesema kuna umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa kuwa hali ya usafi wa mazingira ni mbaya.
Amewataka kusimamia sheria bila woga kwa kuwachukulia hatua watu wanachafua mazingira ikiwemo kutiririsha maji taka hovyo.
"Ni gharama kutibu watu wenye kipindupindu. Mwaka juzi tulikuwa na kambi pale Mburahati na Serikali iliingia gharama kutoa huduma," amesema.
Baadhi ya viongozi wa Serikali za Mitaa wamesema tatizo la mlundikano wa taka linatokana na uhaba wa magari ya taka na madampo.
Katika hatua nyingine, mkuu wa wilaya amewataka kusimamia haki hasa katika suala la ardhi kwa kuwasaidia wanyonge ambao wamedhulumiwa viwanja.