Rais Robert Mugabe amekubali kugeuza kongamano la mwaka la Zanu PFlililopangwa kufanyika Desemba kuwa mkutano mkuu wa congress unaotarajiwa kutumika kumshusha Makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa na kumpaisha mkewe Grace kuwania urais katika chama.
Kamisaa wa Taifa wa Zanu PF Saviour Kasukuwere ndiye aliyependekeza suala la mkutano wa congress alipokuwa anawasilisha ripoti yake kwenye kamati kuu ya chama Jumatano lakini ilibainika kuwa kinara huyo wa kundi la G40 alikuwa amepata ushauri kutoka majimbo matatu tu.
"Mugabe alisema utakuwa ukiukwaji wa taratibu hivyo akaagiza kamati ya maandalizi kuhakikisha ushauri umepatikana kutoka majimbo yote. Kutakuwa na vikao vya uratibu wa majimbo kutafakari suala hilo kuanzia mwishoni mwa wiki hii.
"Mkutano mkuu wa chama umepangwa ili kufanya mabadiliko ya katiba ili kuingiza kifungu cha kuwa na makamu wa rais mwanamke au kuanzisha makamu wa tatu wa rais,” mtu wa ndani alidokeza.
"Suala la urais limekamilika lakini misuguano ya ndani kuhusu kuwania mamlaka na umri wa Mugabe vimelazimisha kutafakari na Nyanja mbalimbali. Kumbuka kuwa Grace anataka madaraka na amekuwa akiomba awe makamu wa rais sambamba na Mnangagwa".
Msemaji wa Zanu PF, Simon Khaya Moyo amekataa kuzungumzia suala hilo.
Miezi miwili iliyopita Mugabe aliwataka wajumbe wa Zanu PF kufikiria kuingiza katika katiba nafasi ya makamu wa tatu wa rais. Hii ilikuwa baada ya mkewe kumtaka kiongozi huyo mkongwe wa Zanu PF kumtangaza mrithi anayempendelea katika mkutano mkuu wa wanawake.