Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya Wafula Chebukati amewashutumu wanasiasa nchini humo akisema wanatatiza maandalizi ya uchaguzi wa marudio Alhamisi wiki ijayo.
Bw Chebukati amesema maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vyema lakini katika mazingira ya sasa ni vigumu kuandaa uchaguzi huru na wa haki iwapo hakutakuwa na mabadiliko.
Amesema pia kwamba maafisa wakuu kwenye tume ya uchaguzi ambao wametajwa kwa njia moja au nyingine kwamba walihusika katika kuvuruga uchaguzi wa kwanza tarehe 8 Agosti wanafaa kujiuzulu.
Bw Chebukati amesema hayo saa chache baada ya mmoja wa makamishna wa wa tume hiyo Dkt Roselyn Akombe kutangaza kujiuzulu akiwa Marekani na kusema hana mipango yoyote ya kurejea Kenya hivi karibuni.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilimtangaza Rais Kenyatta kuwa mshindi wa uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, akiwa mbele ya mpinzani wake Raila Odinga wa muungano wa upinzani Nasa kwa zaidi ya kura 1.4 milioni.
Bw Odinga alipinga matokeo hayo mahakamani na Mahakama Kuu ikaamua ulijaa kasoro nyingi na kuagiza uchaguzi mpya ufanyike katika kipindi cha siku sitini.
Tume ya uchaguzi ilitangaza tarehe mpya ya uchaguzi kuwa 26 Oktoba lakini Bw Odinga alijiondoa wiki iliyopita akisema mageuzi ambayo yalifaa kutekelezwa kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki hayajatekelezwa