Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia, ameondoa kwa muda kusudio lake la kutaka kuwasilisha muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba ya nchi ili kuongeza ukomo wa ubunge.
Nkamia aliwasilisha kusudio hilo Septemba, mwaka huu mjini Dodoma kwa mujibu wa kanuni ya 81(2) ya kanuni za Bunge toleo la 2016, kupitia barua yake aliyoisaini Septemba 12, mwaka huu iliyokuwa ikipendekeza kuongeza muda wa Bunge kutoka miaka mitano hadi saba na kupunguza muda wa uongozi wa vijiji kutoka miaka mitano hadi minne.
Kupitia ujumbe mfupi aliouandika katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp, Nkamia alisema ameamua kuondoa kusudio hilo baada ya majadiliano na maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Ndugu viongozi wenzangu, naomba kuwataarifu kuwa baada ya mashauriano na maelekezo ya viongozi wa juu wa CCM na hali ya kisiasa katika nchi kadhaa za Afrika Mashariki, nimelazimika kuondoa kwa muda hoja yangu binafsi ya ukomo wa Bunge niliyokusudia kuiwasilisha katika Bunge lijalo (linaloanza Novemba, mwaka huu,” aliandika Nkamia.
Hoja ya Nkamia ilianzia Bunge lililopita lakini ilipingwa na wanasiasa wakongwe akiwamo Spika Mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa na wasomi mbalimbali.
Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha Azam, Alhamisi wiki hii, Msekwa alisema CCM haiwezi kukubaliana na maoni ya kuongeza muda wa kiongozi yeyote kutoka kipindi cha miaka mitano kilichopo kwa mujibu wa Katiba ya sasa.
Pia alisema kwa uzoefu wake bungeni anaona kuna tafakuri nyingi zilizofanywa kabla ya Taifa kuamua kipindi cha utawala kuwa miaka mitano na si vinginevyo.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alimpinga huku akisema lengo la Nkamia lilikuwa ni kujipendekeza kwa Rais Dk. John Magufuli ili ampe uwaziri.
Pia Septemba 18, mwaka huu, Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche, alisema anakusudia kuwasilisha bungeni hoja binafsi ili kupunguza muda wa viongozi kukaa madarakani kutoka miaka mitano na iwe minne kama Marekani ili kutoa nafasi kwa wananchi kuwa na uamuzi zaidi wa kuendesha nchi yao.