Kwa sasa Rais anachaguliwa kuongoza nchi kwa miaka mitano, lakini Nkamia anataka uongozwe kuwa miaka saba.
Tayari mbunge huyo alishawasilisha kwa katibu wa Bunge barua ya kutaarifu kuhusu mpango huo ambao iwapo utapita, utaandaliwa muswada wa mabadiliko ya 15 ya Katiba ili uchaguzi uwe unafanyika kila baada ya miaka saba.
Nkamia alisema jana kuwa kesho ataweka hadharani taarifa yake kuhusiana na minong’ono inayoendelea nchini kuwa ameondoa hoja yake.
“Nitazungumza na waandishi wa habari Jumatatu nitaeleza ukweli,” alisema Nkamia alipoulizwa na gazeti hili kuhusiana na uvumi huo wa kuondoa hoja yake.
Miongoni mwa maelezo ya sababu za kutaka marekebisho hayo ni gharama za kuendesha uchaguzi kwa wakati mmoja, yaani Uchaguzi Mkuu na wa serikali za mitaa.
Nkamia alisema hoja yake haimaanishi kuwa Rais aliye madarakani ndiye aanze kwenda miaka saba, bali ni kwa viongozi wote na kama wazo lake likitimia wakati Rais John Magufuli akiwa madarakani nayo si vibaya.
Awali Nkamia alieleza gazeti hili kuwa ataipeleka hoja hiyo katika mkutano wa Bunge wa mwezi Novemba na kwamba anategemewa kuanza maandalizi ya hatua hiyo katika vikao vya kamati za Bunge vilivyofanyika mjini Dodoma.
Lakini hoja hiyo imepingwa na spika wa zamani, Pius Msekwa ambaye alisema wazo hilo lilishajadiliwa na CCM na kuona madhara yake.
Mwanasiasa huyo mkongwe alisema tayari anaona kuna tafakari nyingi zilizofanywa kabla ya Taifa kuamua kipindi cha utawala kuwa miaka mitano na si vinginevyo.
Msekwa alisema hoja hiyo inabidi iangaliwe kwa umakini mkubwa kutokana na ukweli kuwa, iwapo kiongozi atakuwa mbaya, maisha yanaweza kuwa ya mateso kwa wananchi katika kipindi cha miaka saba na kuongeza kuwa hata Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere aliliona hilo.
“Ni kwamba miaka kumi tu inatosha, ili kama mtu ni mbaya tuvumilie kwa hiyo miaka kumi na siyo kwamba haikufikiriwa. Na sidhani kama CCM itakuwa na nafasi ya kujadili hilo kwa sasa,” alisema Msekwa.